Kuna simulizi za maisha ambazo ni nzito kubeba, na ile ya Florence Amunga wa nchini Kenya ni mojawapo. Ni safari iliyojaa maumivu yasiyoelezeka kuanzia utotoni, iliyopitia katika tanuru la moto halisi lililomnyang'anya watoto wake, na kumuacha na makovu ya kudumu mwilini na rohoni. Hata hivyo, ni hadithi ya ajabu ya ujasiri na ari ya kuendelea kuishi.
Safari ya mateso ya Florence ilianza akiwa na umri wa miaka minane tu. Baada ya kifo cha baba yake na mama yake kushindwa kumudu gharama, alilazimika kuingia kwenye ajira za ndani kama mfanyakazi wa nyumbani. "Sikujua kufanya kazi vizuri. Mwajiri wangu wa kwanza alikuwa ananipiga kwa sababu nilishindwa kufua nguo zikang'aa," anakumbuka Florence. Kwa kazi hiyo ya suluba, alilipwa Shilingi 100 za Kenya kwa mwezi (takriban Shilingi 1,500 za Tanzania kwa viwango vya zamani), na hata alipotaka kuacha kutokana na vipigo, mama yake alimlazimisha arejee ili apate fedha hiyo kidogo.
Baada ya kuhangaika katika nyumba mbalimbali, alikimbilia jijini Nairobi kutafuta nafuu, lakini mateso yaliendelea. Ili kukwepa kadhia hiyo, aliamua kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 tu. Alijaliwa kupata watoto wawili na kwa mara ya kwanza akahisi pumziko la maisha. Lakini faraja hiyo haikudumu.
Janga kubwa la maisha yake lilijitokeza wakati wa ghasia za kisiasa zilizoitikisa Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007. Akiwa anaishi katika eneo la Kibera, usiku mmoja watu walichoma nyumba yake huku yeye na wanawe wawili wakiwa wamelala ndani, na kufunga mlango kwa nje.
"Nilichomwamsha ni moshi mzito. Nilijaribu kutoka na wanangu lakini mlango ulikuwa umefungiwa," anasimulia huku akitokwa na machozi. "Wakati napiga mayowe kuomba msaada, mtoto mmoja alikuwa anateketea, mwingine anateketea, na mimi pia nilikuwa nateketea." Katika tukio hilo la kutisha, alimshuhudia mwanawe mmoja akifariki palepale.
Majirani walifanikiwa kuvunja mlango na kuwaokoa, lakini Florence na mwanawe walikuwa wameungua vibaya sana. Walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta. Akiwa hospitalini, alipata pigo la pili. "Nilikaa siku nzima bila kusikia mtoto wangu akilia. Nilipomuuliza daktari, aliniambia alifariki usiku," anakumbuka kwa uchungu.
Katika kipindi hicho kigumu zaidi maishani mwake, mumewe alimtoroka hospitalini na hakurejea tena. Florence alibaki mpweke, akipambana na maumivu ya kuungua mwili na maumivu ya kupoteza familia yake. Alifanyiwa upasuaji mara kumi ili kurekebisha ngozi yake, huku madaktari wakitumia ngozi kutoka sehemu nyingine za mwili wake "kumziba viraka". Majeraha yalikuwa makubwa kiasi kwamba alipoteza masikio yake.
Licha ya kupitia yote hayo, Florence amesimama tena. Alipata ushauri nasaha uliomsaidia kukubali hali yake. Baadaye alipata mume mwingine na kujaliwa watoto watatu, ingawa kwa bahati mbaya, mume huyo naye alifariki dunia kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (COVID-19). Leo, Florence anaendelea na maisha, akiwa na matumaini ya kupata wahisani watakaomsaidia kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa masikio bandia, akiwa ni ushuhuda hai wa nguvu ya roho ya mwanadamu.