Tukio la kushangaza limetokea katika kijiji cha Kuchimuchi, jimbo la Uttar Pradesh nchini India, ambapo bwana harusi mwenye umri wa miaka 75, Sangruram, amefariki dunia ghafla siku moja tu baada ya kufunga ndoa na mwanamke mwenye umri wa miaka 35, Manbavati. Kifo hicho kimezua maswali mengi, na kusababisha ndugu wa marehemu kuingilia kati na kutaka uchunguzi ufanyike.
Sangruram, ambaye alikuwa mkulima kutoka jamii ya Dalit (jamii ya matabaka ya chini), alikuwa akiishi peke yake kwa takriban mwaka mmoja baada ya kufiwa na mke wake wa kwanza. Kwa kuwa hakuwa na watoto, aliamua kutafuta mwenza wa kumfariji katika maisha yake, ndipo alipokutana na Manbavati, mjane mwenye watoto watatu ambaye pia alikuwa amefiwa na mumewe miaka saba iliyopita.
Wawili hao walifanya maamuzi ya kuoana na mnamo tarehe 29 Septemba, walifanikisha ndoa yao kisheria katika mahakama ya eneo hilo na baadaye kufanya sherehe za jadi hekaluni. Kulingana na Manbavati, usiku wao wa kwanza ulikuwa wa furaha na walizungumza mengi. Mumewe alimuahidi kuwa angewatunza watoto wake kama wake, huku akimtaka yeye asimamie shughuli za nyumbani.
Hata hivyo, furaha ya ndoa hiyo haikudumu. Asubuhi iliyofuata, Sangruram alimwamsha mkewe kama kawaida na alionekana mwenye afya njema. Ghafla, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya, akalegea na kulala kitandani. Licha ya juhudi za mkewe kumtafutia daktari na kumkimbiza hospitalini kwa msaada wa majirani, alitangazwa kuwa amefariki dunia alipofika hospitali.
Habari za kifo hicho zilipomfikia mpwa wa Sangruram anayeishi mji mkuu wa Delhi, takriban kilomita 500 kutoka kijijini, aliingilia kati haraka. Alipiga simu na kuzuia mwili wa mjomba wake usichomwe moto, akisisitiza ufanyiwe uchunguzi wa kina (autopsy) ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake.
Manbavati anasisitiza kuwa mumewe alikuwa buheri wa afya kabla ya mauti kumkuta. Alifichua pia kuwa marehemu alimwahidi kuwa angemwandikisha kama mrithi wa mali zake zote, na alikuwa ameshatenga kiasi cha Rupia 100,000 (takriban Shilingi milioni 3.1 za Kitanzania) kwa ajili ya kila mmoja wa watoto wake watatu.