Kampuni kubwa ya biashara ya rejareja nchini Marekani, Target, imetangaza hatua ya kihistoria na ya kushtua ya kupunguza maelfu ya wafanyakazi wake, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja (miaka 10) kwa kampuni hiyo kufanya uamuzi mkali kiasi hicho.
Kwa mujibu wa tangazo rasmi, takriban wafanyakazi 1,800 wa makao makuu ya kampuni hiyo watapoteza ajira zao, hatua ambayo ni sawa na kupunguza asilimia 8 ya wafanyakazi wote wa ngazi ya ofisi kuu. Msemaji wa Target alihakikisha kuwa wafanyakazi wa mstari wa mbele, yaani wale wanaohudumu katika maduka na vituo vya usambazaji (maghala), hawataathiriwa na uamuzi huu.
Tangazo hili lilitolewa kupitia barua ya ndani kwa wafanyakazi iliyoandikwa na Bosi Mkuu Mtarajiwa, Bw. Michael Fideleke. Bw. Fideleke, ambaye kwa sasa ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji (COO) na anatarajiwa kuchukua rasmi wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji (CEO) mnamo Februari 1 mwaka ujao, alieleza sababu za uamuzi huo mgumu.
Kwenye barua yake, Fideleke alisema kampuni imekuwa na "muundo mgumu" na urasimu uliokithiri ambao umekuwa kikwazo kwa ubunifu na kasi ya utendaji. "Urasimu ambao tumejijengea kwa miaka mingi sasa unatukwamisha," aliandika Fideleke. Alifafanua kuwa kuwepo kwa "tabaka nyingi za uongozi na majukumu yanayoingiliana" kumesababisha maamuzi kufanywa kwa polepole sana, na kufanya iwe vigumu kwa mawazo mazuri kutekelezwa kwa haraka.
Alikiri kuwa upunguzaji huu wa wafanyakazi ni "mchakato mgumu na unaoumiza," lakini akasisitiza kuwa ni hatua "isiyoepukika" na ndiyo "hatua ya kwanza katika kuijenga upya Target kwa siku zijazo." Mpango huu unajumuisha kuwafuta kazi moja kwa moja wafanyakazi 1,000, huku nafasi zingine 800 zilizokuwa wazi zikifutwa (hazitaajiriwa tena).
Kwa nini Target imefikia hatua hii? Kampuni hii kubwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa kwa miaka minne mfululizo. Imeshuhudia mauzo yake yakiganda (stagnant sales), wateja wengi wakiikimbia, matatizo ya usimamizi wa hesabu za bidhaa (inventory), na hata malalamiko ya wateja kuhusu mabadiliko ya kuongeza mashine za kujihudumia (kiosks) madukani.
Hali ni mbaya kiasi kwamba kampuni hiyo imetabiri rasmi kuwa mauzo yake ya mwaka huu yatashuka. Hii imeathiri moja kwa moja thamani ya kampuni kwenye soko la hisa. Thamani ya hisa za Target imeporomoka kwa asilimia 65 tangu ilipofikia kilele chake mwishoni mwa mwaka 2021.
Wakati Target ikiporomoka, mshindani wake mkuu, Walmart, anazidi kung'ara. Takwimu za miaka mitano iliyopita zinaonyesha picha halisi: hisa za Walmart zimepanda kwa asilimia 123%, huku hisa za Target zikishuka kwa asilimia 41% katika kipindi hicho.
Wataalamu wa soko la rejareja wanaeleza kuwa chanzo kikuu cha tofauti hii ni aina ya bidhaa wanazouza. Walmart imejikita zaidi kwenye "bidhaa za lazima" (essentials); takriban asilimia 60 ya mauzo yake yote ni vyakula na mahitaji ya kila siku ya nyumbani. Kinyume chake, Target inategemea zaidi "bidhaa za anasa" au zisizo za lazima (non-essentials). Zaidi ya nusu ya mauzo ya Target ni nguo na vifaa vya mapambo ya nyumbani. Katika hali ya sasa ya uchumi duniani ambapo gharama za maisha zimepanda, wateja wengi wanabana matumizi na kuelekeza fedha zao kwenye mahitaji ya msingi (chakula) badala ya nguo mpya au mapambo.
Bosi huyu mpya, Fideleke, ambaye aliwahi kuwa Afisa Mkuu wa Fedha (CFO), anaonekana kuletwa mahsusi kusafisha hali hii. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa akiongoza ofisi mpya iliyoanzishwa Mwezi Mei, iitwayo "Ofisi ya Kuharakisha Ukuaji wa Biashara," iliyopewa jukumu la kurahisisha utendaji, kuongeza matumizi ya teknolojia, na kuharakisha ukuaji.