Hali ya wasiwasi imeongezeka nchini Kenya baada ya Rais William Ruto kutoa agizo tata kwa jeshi la polisi, akiwataka kutumia nguvu kuzima maandamano yanayoendelea kwa kuwapiga risasi za miguu waandamanaji wanaohusika na uharibifu wa mali. Kauli hii ya rais imekuja wakati tayari taifa hilo jirani linakabiliwa na mzozo mkubwa uliosababisha vifo vya makumi ya watu.
Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Ruto alisisitiza kuwa polisi hawapaswi kuua waandamanaji, lakini badala yake wanapaswa "kuwapiga risasi miguuni na kuwapeleka hospitali" wale wanaochoma au kuharibu mali za watu. Alionya vikali, akisema kuwa mtu yeyote anayeshambulia polisi, vituo vya polisi, au miundombinu ya usalama anatangaza vita na anafanya kitendo cha ugaidi. "Taifa haliwezi kuendeshwa na magaidi au kutawaliwa na ghasia. Tutachukua hatua madhubuti," alionya Ruto, akiongeza kuwa nchi haitaruhusu kuharibiwa na wachache wanaotaka kubadilisha serikali kwa njia zisizo za kikatiba.
Agizo hili la Rais Ruto limetolewa siku moja tu baada ya Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC) kutangaza takwimu za kutisha. Tume hiyo iliripoti kuwa watu 31 wameuawa, 107 wamejeruhiwa, na takriban 530 wamekamatwa kutokana na ukandamizaji mkali wa polisi dhidi ya waandamanaji. Kwa ujumla, idadi ya vifo vilivyotokana na maandamano katika wiki mbili zilizopita imefikia watu 50, ikijumuisha vifo 19 vilivyotokea wakati wa maandamano makubwa ya kupinga ongezeko la kodi mnamo Juni 25.
Tume ya Haki za Binadamu imelaani vikali matumizi ya nguvu kupita kiasi na imedai kuwa kuna ushahidi unaoonyesha polisi walishirikiana na magenge ya wahalifu wakati wa operesheni zao za kuzima maandamano. "Tunalaani ukiukwaji wote wa haki za binadamu na tunatoa wito kwa wahusika wote, wakiwemo polisi na raia, kuwajibika kwa matendo yao," ilisema taarifa ya tume.
Maandamano nchini Kenya yamekuwa yakishika kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na hasira ya umma juu ya masuala kadhaa, ikiwemo nyongeza ya kodi, ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana, ukatili wa polisi, na ufisadi uliokithiri miongoni mwa viongozi wa serikali. Mnamo Julai 7, maelfu ya raia walijitokeza tena katika miji mbalimbali, ikiwemo mji mkuu Nairobi, kupinga masuala hayo. Tarehe hii ina umuhimu wa kihistoria, kwani ni kumbukumbu ya "Saba Saba", maandamano makubwa ya mwaka 1990 yaliyodai kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo.