Rais wa Kenya, Dk. William Ruto, amewataka wapinzani wake kuzingatia Katiba na kutafuta suluhisho la changamoto za nchi kupitia mikakati thabiti badala ya kushinikiza yeye aondoke madarakani kupitia maandamano. Akizungumza jijini Nairobi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Biashara Ndogo na za Kati Duniani (SMEs), mwaka 2025, Rais Ruto alisisitiza kuwa Katiba ya Kenya inaweka wazi kipindi cha urais, hivyo mjadala kuhusu "muhula mmoja tu" (wantam) hauna msingi.
Katika hotuba yake kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC), Rais Ruto alipinga vikali wito wa wapinzani wa kutaka ajiuzulu, akifafanua kuwa wanapaswa kuja na mpango mbadala wa kuwaongoza Wakenya badala ya kauli mbiu za 'Ruto lazima aondoke'. "Ikiwa mnamaanisha Ruto lazima aondoke, niambieni mnataka niondoke vipi? Tuna Katiba," alisema Ruto, akiongeza kuwa njia sahihi ni kushawishi wananchi kwa sera bora zitakazowafanya wamchague kiongozi mwingine. Aliongeza kuwa, kama wapinzani watamshawishi mwananchi wa kawaida wa Kenya kuwa na mpango mbadala na bora zaidi, yeye (Ruto) ataondoka madarakani na kujikita katika kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Rais Ruto pia alikemea vikali maandamano yaliyokumba Nairobi na maeneo mengine nchini, akisisitiza kuwa hayakuwa ya amani bali yalikuwa ni vitendo vya ghasia, uporaji, uharibifu wa mali, na hujuma dhidi ya uchumi wa taifa. "Kile tulichoshuhudia hakikuwa maandamano ya amani, bali ilikuwa ni fujo zilizopangwa, vurugu, na uharibifu," alisisitiza Rais, akitoa agizo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale wote waliohusika na vitendo hivyo.
Akionesha huruma kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na wafanyabiashara walioathirika, Ruto alionya kuwa vurugu na uharibifu wa biashara, vikiachwa viendelee, vinaweza kuenea nchini kote na kuhatarisha maisha ya kila mmoja. Alihitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa kutumia njia za heshima na kistaarabu za kutafuta uongozi, akisisitiza umuhimu wa kuwasilisha mipango bora kwa wananchi badala ya kuibiana nchi na kuiingiza katika machafuko.