EACOP Yapeta Tena Arusha: Mahakama ya EACJ Yawatupa Nje Wanaharakati, Mradi Kusonga Mbele

international | Thu Nov 27 2025


EACOP Yapeta Tena Arusha: Mahakama ya EACJ Yawatupa Nje Wanaharakati, Mradi Kusonga Mbele

Jitihada za mashirika ya kiraia (CSOs) kutoka nchi za Afrika Mashariki kukwamisha ujenzi wa Mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) zimegonga mwamba kwa mara ya pili mfululizo. Hii ni baada ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) yenye makao yake jijini Arusha, kutupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na mashirika hayo kupinga utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria.


Hukumu hiyo iliyotolewa jana, Novemba 26, 2025, na jopo la Majaji watano wakiongozwa na Jaji Nestor Kayobera, imekuwa kama 'maji ya baridi' kwa mashirika manne yaliyoongoza jahazi hilo la kisheria ambayo ni Center For Food And Adequate Living Rights (CEFROHT), African Institute For Energy Governance (AFIEGO), Natural Justice Kenya na Center For Strategic Litigation Limited (CSL).


Sababu za Kisheria: "Mlchelewa Kufika" Katika shauri hilo la rufaa namba 4 la mwaka 2023, majaji wa EACJ wamekubaliana na hoja za wajibu maombi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Uganda, na Katibu Mkuu wa EAC) kwamba kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda uliowekwa kisheria. Hii inamaanisha kuwa mahakama haikuweza kusikiliza hoja za msingi (substantive arguments) kuhusu mazingira na haki za binadamu, bali ilijikita katika vigezo vya kisheria vya muda wa ufunguaji kesi.


Uamuzi huu unatoa nafasi kwa serikali za Tanzania na Uganda kuendelea na utekelezaji wa mradi huo wa kilomita 1,443 kutoka Hoima (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania), mradi unaotegemewa kubadili sura ya uchumi wa ukanda huu.


Wanaharakati Wafunguka kwa Masikitiko Akizungumza kwa hisia nzito nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo, Mwanasheria wa Mazingira kutoka Shirika la Center for Strategic Litigation (CSL), Noel Mdoe, alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo. Alidai kuwa mahakama imetumia "kisingizio cha muda" kukwepa kujadili hoja nzito zinazogusa maisha ya watu na uharibifu wa mazingira.


"Inasikitisha sana. Tulikuja hapa na matumaini makubwa kuwa chombo hiki cha haki cha Jumuiya yetu kingetupa sikio. Hoja zetu zilijikita kwenye ukweli kwamba mikataba ya mradi huu (IGA na HGA) ilisainiwa kinyume cha taratibu. Kwa mfano, mkataba wa IGA kati ya Tanzania na Uganda ulisainiwa mwaka 2017, wakati tathmini ya athari za mazingira (ESIA) ilikuja kupitishwa mwaka 2020. Huwezi kusaini mkataba kabla hujajua athari za mazingira," alilalamika Mdoe.


Hata hivyo, Mdoe ameapa kuwa hawataishia hapo. "Safari bado ni mbichi. Tutarejea mezani na wadau wetu kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua nyingine za kisheria, iwe ni katika mahakama za kikanda au za kimataifa, kwa ajili ya maslahi mapana ya Afrika Mashariki."


Kilio cha Fidia na Mfumuko wa Bei Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la OCE (Organization For Community Engagement Tanzania), Richard Senkondo, aliibua hoja ya kiuchumi inayowagusa wananchi wa kawaida. Alibainisha kuwa ucheleweshaji wa fidia umewasababishia umaskini wananchi waliopisha mradi huo.


"Fikiria ardhi ilifanyiwa tathmini mwaka 2018, lakini fidia imekuja kulipwa kati ya mwaka 2022 na 2023. Huu ni mkupuo wa takriban miaka mitano. Katika kipindi hicho, thamani ya ardhi ilipanda, na mfumuko wa bei uliongezeka. Fedha waliyolipwa mwaka 2023 haiwezi kununua ardhi yenye ukubwa sawa na ile waliyopoteza mwaka 2018. Wengi walizuiwa kulima kwa muda mrefu, hivyo wamepoteza uwezo wa kuzalisha mali," alifafanua Senkondo.


Licha ya changamoto hizo za kisheria, Serikali za Tanzania na Uganda zimeendelea kushikilia msimamo kuwa EACOP ni mradi muhimu kwa uchumi, na kwamba tahadhari zote za kimazingira na haki za binadamu zimezingatiwa kwa viwango vya kimataifa.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.