Serikali ya China imechukua hatua kubwa ya kusisimua uchumi wake kwa kuzindua sera mpya inayolenga kuongeza matumizi ya kifedha miongoni mwa wananchi wake. Sera hiyo inajumuisha ruzuku ya riba kwa mikopo ya matumizi, hatua inayotarajiwa kuwahamasisha watu kutumia zaidi. Wizara ya Fedha ya China, Benki ya Watu wa China, na mamlaka ya usimamizi wa fedha wametangaza rasmi mpango huu ambao utaanza kutekelezwa tarehe 1 Agosti, 2024, hadi 31 Agosti, 2025.
Chini ya mpango huu, mtu yeyote atakayechukua mkopo wa matumizi binafsi kutoka kwa taasisi za kifedha zilizoidhinishwa na kuthibitishwa kuwa fedha hizo zimetumika kwa madhumuni ya matumizi, atapata punguzo la riba. Hata hivyo, kuna vigezo maalum. Punguzo hili litatolewa kwa mikopo yenye thamani isiyozidi Yuan 50,000 (sawa na takriban TZS 17.5 milioni), au kwa mikopo ya matumizi makubwa katika sekta muhimu kama vile ununuzi wa magari binafsi, huduma za wazee, uzazi, elimu, utalii, ukarabati wa nyumba, vifaa vya kielektroniki, na huduma za afya. Hata kama mtu atachukua mkopo mkubwa zaidi ya Yuan 50,000, punguzo la riba litatumika tu kwenye kiwango cha juu cha Yuan 50,000.
Kuhusu kiwango cha punguzo la riba, serikali imeweka ukomo wa asilimia 50 ya riba ya mkataba wa mkopo, lakini punguzo la juu kabisa lisizidi asilimia 1 kwa mwaka. Aidha, jumla ya punguzo la riba kwa mkopo wa matumizi kwa mtu mmoja halitazidi Yuan 3,000 (takriban TZS 1.05 milioni) kwa kipindi chote cha utekelezaji wa sera. Gharama za ruzuku hii zitagawanywa kati ya serikali kuu na serikali za mikoa, ambapo serikali kuu itabeba asilimia 90 na serikali za mikoa asilimia 10.
Taasisi za mikopo zitakazohusika katika mpango huu ni pamoja na benki sita kubwa za kibiashara zinazomilikiwa na serikali, benki 12 za kibiashara za hisa, na taasisi nyingine tano za kutoa mikopo ya matumizi binafsi. Kulingana na Naibu Waziri wa Fedha, Liao Min, hii ni mara ya kwanza kwa serikali kuu ya China kutoa ruzuku ya riba moja kwa moja kwa mikopo ya matumizi ya wananchi, akisisitiza kuwa sera hii italeta manufaa makubwa kwa wananchi wengi. Alisema pia kuwa serikali itafuatilia utekelezaji wake na inaweza kuongeza muda wa sera hiyo baada ya mwaka mmoja kulingana na matokeo. Mamlaka hizo zimeonya kuwa udanganyifu wowote utakaobainika katika mchakato wa uthibitishaji wa matumizi utashughulikiwa kisheria, na ruzuku hiyo itarejeshwa.