Benki Kuu ya Afrika Kusini (SARB) imepunguza kiwango cha riba ya benki kwa pointi 25 za msingi, na kufanya riba sasa kuwa asilimia 7.00%. Uamuzi huu, uliotolewa na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC), ni mara ya pili mfululizo kufanya punguzo kama hilo, na ni kiwango cha chini kabisa cha riba tangu Novemba 2022.
Gavanya wa Benki Kuu, Lesetja Kganyago, alitoa ufafanuzi kwamba hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kushuka kwa kasi ya mfumuko wa bei hivi karibuni. Alisema hali hii imeiimarisha sarafu ya nchi hiyo, Rand, na kupunguza gharama za mikopo ya muda mrefu. Kganyago alisisitiza umuhimu wa kudumisha hali hii na kupunguza sintofahamu kuhusu malengo ya sera ya fedha ya muda mrefu. Aliongeza kuwa uamuzi wa kupunguza riba ulipitishwa kwa kura za wajumbe wote wa MPC.
Kupunguzwa kwa riba kunaweza kuonekana kama hatua ya kulinda uchumi wa ndani, hasa ikizingatiwa kuwa inakuja siku moja kabla ya Marekani kuweka ushuru mpya wa asilimia 30 kwa bidhaa za Afrika Kusini. Gavana Kganyago alikuwa ametoa onyo hapo awali kwamba hatua hiyo ya Marekani inaweza kuhatarisha nafasi za ajira 100,000 na kuathiri vibaya sekta za kilimo na magari.
Kuhusu athari za uchumi wa kimataifa, Kganyago alisema Benki Kuu imeshusha utabiri wake wa ukuaji wa uchumi wa mwaka huu kutokana na ushuru mpya kutoka Marekani. Hata hivyo, alieleza matumaini yake kuwa ukuaji wa uchumi wa wastani utaendelea kwa miaka ijayo kutokana na maboresho ya kiuchumi yanayoendelea nchini humo.