Wafugaji wa Vizimba Mwanza Waililia Serikali: Bila Ruzuku Kwenye Chakula, Ufugaji Ni Mgumu

economy | Tue Sep 16 2025


Wafugaji wa Vizimba Mwanza Waililia Serikali: Bila Ruzuku Kwenye Chakula, Ufugaji Ni Mgumu

Jitihada za serikali za kukuza uchumi wa bluu na kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba mkoani Mwanza, zinakabiliwa na kikwazo kikubwa: gharama kubwa za chakula cha samaki. Sasa, wafugaji hao wanaiomba serikali kuingilia kati kwa kuweka ruzuku kwenye vyakula hivyo ili kuwapunguzia mzigo na kufanya shughuli zao kuwa endelevu.


Akizungumza Jumanne iliyopita kwa niaba ya wenzake, Fikiri Elias, Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha Imani Aqua Farm, alisema ingawa mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imewapa mwanzo mzuri, faida yao inayeyuka kutokana na bei ya juu ya chakula. Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama zote za uendeshaji wa mradi wa vizimba inaishia kwenye ununuzi wa chakula pekee.


"Tunaishukuru serikali kwa mikopo, lakini tunaiomba itazame upande wa pili wa sarafu. Kama ilivyo kwenye mazao ya kilimo ambapo kuna ruzuku, tunaomba na sisi katika sekta ya uvuvi tupate ruzuku kwenye chakula cha samaki. Hii itapunguza gharama na kutuwezesha kushindana sokoni," alisema Elias.


Ufanisi wa awali wa miradi hii unaonesha jinsi gani vijana wamechangamkia fursa. Elisha Abel wa kikundi cha Vijana Kazini anasimulia jinsi mkopo wa Shilingi milioni 117 ulivyowawezesha kuanzisha vizimba na kununua vifaranga. "Katika mavuno yetu ya kwanza, tulivuna tani 13 za samaki na kupata zaidi ya Shilingi milioni 101, tukarejesha sehemu ya mkopo na kuendeleza mradi. Mafanikio haya yapo," alisema Abel.


Hata hivyo, Abel anasisitiza kuwa gharama za sasa za chakula zinaweza kukwamisha ndoto zao. "Chakula cha kuanzishia vifaranga, yaani 'starter', kinauzwa hadi Shilingi 4,500 kwa kilo. Hii ni bei kubwa sana. Tunaomba serikali itusaidie kupunguza bei ili tuweze kuzalisha zaidi na kuajiri vijana wengi zaidi," aliongeza.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo kutoka TADB, Glacia Marugujo, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya gharama. Alisema benki hiyo inaendelea na mazungumzo na wadau, ikiwemo viwanda vinavyozalisha chakula cha samaki, ili kutafuta njia ya kupunguza bei na kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora na cha bei nafuu kwa wafugaji wanaowezeshwa na serikali.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.