Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng'i Issa, ameonesha masikitiko yake kutokana na hali ya vijana nchini kutokuwa na mwitikio chanya katika kuchangamkia fursa za mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali. Amesema hali hii inasababisha vijana wengi kuendelea kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Bi. Beng'i aliyasema hayo jana jijini Mwanza katika kongamano lililoandaliwa na kampuni ya Victory Business Consultant, ambalo liliwaleta pamoja wanawake na vijana kujadili masuala ya uwezeshaji kiuchumi.
Alibainisha kuwa kwa sasa, wanawake ndio wanaongoza kwa kuchukua na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati, tofauti na vijana ambao wengi wao wanahitaji mitaji kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara zao.
Bi. Beng'i alisema kuwa tatizo hilo linatokana na ukosefu wa taarifa sahihi zinazowafikia vijana kuhusu fursa hizo za mikopo. Hali hii inawafanya wengi wao wasijue wapi wanaweza kupata mikopo hiyo yenye masharti nafuu.
"Mpango wa halmashauri wa asilimia 10, ukiangalia fedha zinazotolewa kwa mwaka na halmashauri zote nchini, zinafikia zaidi ya Shilingi bilioni 80 hadi 100 za Kitanzania. Sasa, ukichukua asilimia nne ya fedha hizo ambazo vijana wanatakiwa kuchukua, ni karibu Shilingi bilioni 40, lakini hawachukui. Mara nyingi hawafikii hata Shilingi bilioni 20," alieleza Bi. Beng'i.
Aliongeza kuwa serikalini kuna programu nyingi zinazolenga kuwasaidia vijana kupata mitaji, ikiwemo mifuko zaidi ya 20 inayotoa mikopo. Kati ya mifuko hiyo, 14 inatoa mikopo kupitia benki kwa dhamana ya Serikali. Hata hivyo, aliwatahadharisha vijana wanaochukua mikopo na kukimbia bila kulipa, akisisitiza kuwa mfumo umekuwa wa kisasa na wanaweza kubainika kwa urahisi.
"Tupo 'connected' (tumeunganishwa). Ukichukua mkopo kwenye simu, inajulikana wewe umechukua mkopo. Ukienda kuchukua mkopo benki na tayari una mkopo kwenye simu, wanajua. Wewe katika maisha yako ya ujanja ujanja, mtu akitaka kukulipa kwenye biashara yako akakuambia nakulipa kwa namba ya simu au nakutumia pesa, unamwambia asitumie hiyo namba, tumia nyingine. Unaogopa ule mkopo wako utakatwa, lakini ipo siku utashikwa," alionya Bi. Beng'i.
Aliwashauri vijana wanaotamani kujiajiri kwa kufanya ujasiriamali kuweka uaminifu mbele katika biashara zao. Alisema kwa kufanya hivyo, watafanikiwa bila lazima kukopa, hasa kama hawana uhakika wa matumizi sahihi ya mikopo hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Victory Business Consultant, Bw. Albert Gilenga, alisema kuwa kongamano hilo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii. Zaidi ya vijana 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa walikutana kujadili na kutafuta suluhu kwa changamoto zao, pamoja na kuoneshwa fursa zinazopatikana serikalini na katika sekta binafsi.
"Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana na wanawake. Hawa pia ndio wanaoshiriki sana katika shughuli za biashara na ndio kundi lililo katika uzalishaji. Tuliona tukiwawezesha vijana na wanawake kwa kutatua changamoto zao na kuwaonesha fursa zinazotolewa na Serikali na sekta binafsi, tunaweza kuwa tumefanya mchango mkubwa kwa jamii," alisema Bw. Gilenga.
Naye Mkurugenzi wa Mipango wa kampuni hiyo, Dkt. Boniphace Nyabweta, alishauri idara za maendeleo ya jamii kuanzia ngazi ya kata kuhakikisha zinawafikishia vijana taarifa kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana serikalini, kwani wengi wao hawana uelewa nazo.
"Jambo kama hilo halifanyiki ipasavyo. Tuiombe Serikali, kupitia makongamano kama haya, waone namna gani maofisa maendeleo wanashuka kuwafikia vijana na kuwapatia hizo taarifa za fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali," alisisitiza Dkt. Nyabweta.