Afrika Kusini Yajibu Hatua ya Marekani Kumfukuza Balozi Wake

international | Sat Mar 15 2025


Afrika Kusini Yajibu Hatua ya Marekani Kumfukuza Balozi Wake

Serikali ya Afrika Kusini imesema kuwa uamuzi wa Marekani kumfukuza balozi wake ni wa kusikitisha, huku ikisisitiza haja ya kuheshimu misingi ya kidiplomasia katika kushughulikia masuala yanayohusu mataifa mawili hayo.


Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kutangaza kuwa balozi wa Afrika Kusini nchini humo, Emrahim Rasool, ni persona non grata (mtu asiyetakiwa), akimtuhumu kwa ubaguzi wa rangi.


Afrika Kusini imeeleza kuwa bado inathamini uhusiano wake na Marekani na itaendelea kushirikiana na taifa hilo kwa maslahi ya pande zote mbili.


Chanzo cha Mzozo wa Kidiplomasia

Mzozo huu wa kidiplomasia umechochewa na matamshi ya Balozi Rasool, ambaye aliripotiwa kukosoa utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa madai kuwa aliongoza harakati za kuhimiza ubaguzi wa rangi duniani. Matamshi hayo yaliibuliwa na Waziri Rubio, aliyewashutumu viongozi wa Afrika Kusini kwa maoni hayo kupitia mitandao ya kijamii.


Tangu Trump aondoke madarakani, mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Afrika Kusini umeendelea, hasa kuhusu masuala ya ardhi na haki za binadamu. Trump aliwahi kushutumu serikali ya Afrika Kusini kwa kuchukua ardhi kutoka kwa wakulima wazungu, madai ambayo serikali ya Afrika Kusini imeyakanusha mara kwa mara.


Hivi karibuni, Trump alitangaza kutoa uraia kwa wakulima wa Afrika Kusini wanaotaka kuhama nchini humo, hatua inayoweza kuongeza mvutano kati ya mataifa haya mawili.


Afrika Kusini imeitaka Marekani kuzingatia staha ya kidiplomasia katika kushughulikia masuala ya aina hii na kuendelea kujenga mahusiano yenye tija badala ya kuyaathiri kwa maamuzi ya haraka.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.