Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ametangaza kuwa balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani, Ebrahim Rasool, hatakaribishwa tena nchini humo na atafukuzwa kama "persona non grata" (mtu asiyehitajika kidiplomasia).
Kwa mujibu wa taarifa za CNN, Rubio aliandika kwenye mtandao wa kijamii X (zamani Twitter) kwamba "Balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani si mtu anayetakiwa tena katika taifa letu kubwa."
Rubio alimshutumu Rasool kwa madai ya kutoa matamshi yenye chuki dhidi ya Marekani na Rais Donald Trump. "Hatuwezi kuwa na mjadala wowote naye, na kwa hivyo, tunamchukulia kama mtu asiyehitajika kidiplomasia," aliandika Rubio.
Katika chapisho lake, Rubio aliambatanisha kiungo cha makala inayomnukuu Rasool akimkosoa Trump kwa kile alichokiita "uongozi wa harakati za Marekani kwa ajili ya ubabe wa taifa hilo duniani."
Hatua ya Marekani kumfukuza balozi wa taifa jingine ni jambo lisilo la kawaida na linaweza kuzua mvutano wa kidiplomasia kati ya Washington na Pretoria.
Rubio alitoa tangazo hilo akiwa safarini kurejea Marekani baada ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani (G7) uliofanyika Quebec, Canada.
Mwezi uliopita, Rais Trump alisaini agizo la kusitisha msaada kwa Afrika Kusini, akipinga sera ya serikali ya nchi hiyo kuhusu utaifishaji wa ardhi, akidai kuwa ni ya kibaguzi.