Wakati Kampuni ya Sukari ya Kilombero (KSCL) ikijiandaa na mradi mkubwa wa upanuzi wa kiwanda chake unaofahamika kama 'K4', jumla ya wakulima 734 wa miwa kutoka vyama 17 vya ushirika (AMCOS) wamehitimu mafunzo maalum ya kuongeza tija, wakiandaliwa kunufaika na fursa kubwa ya kiuchumi inayokuja.
Mafunzo hayo, yanayojulikana kama Mpango wa Elimu Tija, yameendeshwa na Taasisi ya Kilombero Community Charitable Trust (KCCT) kwa udhamini mkuu wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero. Lengo ni kuwapa wakulima ujuzi wa kisasa utakaowawezesha kuongeza mavuno na ubora wa miwa yao, na hivyo kuongeza kipato chao.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya KCCT, Derick Stanley, alisema mafunzo haya yamekuja wakati muafaka. "Mradi wa upanuzi wa K4 utaongeza uhitaji wa miwa kwa kiasi kikubwa sana. Wakulima hawa sasa wana maarifa ya kutumia fursa hii kikamilifu. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuungana nasi kuwawezesha wakulima wa Kilombero," alisema Stanley.
Programu hiyo ya mafunzo iliwapa wakulima ujuzi katika maeneo makuu matano: mbinu bora za kilimo cha kisasa, usimamizi wa fedha, ujasiriamali, na utunzaji wa mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kilombero Sugar, Guy Williams, aliwapongeza wahitimu na kusisitiza kuwa kampuni yake itaendelea kuwa mshirika mkuu wa wakulima na jamii ya Kilombero, kama ilivyofanya kwa zaidi ya miaka 25 kupitia KCCT.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Pilly Kitwana, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, aliipongeza KCCT na Kilombero Sugar kwa kuwawezesha wakulima. "Mafunzo haya ni msingi imara wa mabadiliko ya kweli katika maisha ya wananchi wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuleta maendeleo," alisema Kitwana.
Kwa upande wao, wakulima waliohitimu walishukuru kwa kupata maarifa hayo na kuomba programu iendelezwe kwa kuongeza mashamba darasa ili waweze kujifunza kwa vitendo zaidi, na hivyo kuwa tayari kikamilifu kwa mapinduzi ya kilimo cha miwa yanayokuja katika Bonde la Kilombero.