Habari njema kwa wakulima na sekta ya kahawa nchini ni kwamba Umoja wa Ulaya (EU) unafikiria kuanzisha kituo maalum cha mafunzo ya zao hilo, hatua inayolenga kuwajengea uwezo na kuongeza ujuzi hasa kwa wakulima wadogo. Mpango huu muhimu umedokezwa kufuatia ziara ya mabalozi 12 wa nchi wanachama wa EU mkoani Kilimanjaro, waliofika kujionea mnyororo mzima wa thamani wa zao la kahawa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Balozi wa Italia nchini, Giuseppe Coppola, alisema lengo la ziara yao iliyofanyika katika Wilaya ya Moshi ni kuelewa kwa undani fursa na changamoto zilizopo ili kubaini maeneo mahususi ya kusaidia. Baada ya mazungumzo na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) na kutembelea shamba la kisasa la Kilimanjaro Plantation, mabalozi hao walivutiwa na ubora na mbinu za kisasa zinazotumika nchini.
"Tumejifunza mambo mengi kuanzia upandaji hadi uzalishaji katika shamba hili. Tumefurahishwa na jinsi kazi zinavyofanyika kisasa na ubora wa kahawa inayozalishwa Tanzania. Hii inatupa msukumo wa kuunga mkono mradi wa kuanzisha kituo cha mafunzo ili kueneza teknolojia hii kwa wakulima wengi zaidi," alisema Balozi Coppola.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo, alieleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kibiashara na Ulaya, ambalo ndilo soko kubwa zaidi la kahawa ya Tanzania, linalonunua asilimia 50 ya uzalishaji wote. "Tumewahakikishia wenzetu kuwa Tanzania inazalisha kahawa endelevu isiyotokana na uharibifu wa misitu, jambo ambalo ni sharti muhimu katika soko la Ulaya," alibainisha Kimaryo.
Ili kuthibitisha hili, Mkurugenzi wa Kilimanjaro Plantation, Colton Rebenold, aliwaeleza mabalozi jinsi shamba lake lenye miti milioni 1.2 linavyotumia mbolea ya asili inayotengenezwa kwa minyoo (vermicompost) ili kulinda mazingira na kukidhi vigezo vya masoko ya kimataifa, hasa Ulaya, Marekani na Japan.