Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, ametoa wito kwa Chama cha Watoa Huduma katika Sekta ya Madini (TAMISA) kuhakikisha wanachama wao wanakuwa waaminifu na kudhibiti wale wachache wasiokuwa na uadilifu. Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA, Mhandisi Samamba alisisitiza kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo sasa katika sekta ya madini ni fursa adhimu ambayo inapaswa kutumiwa na wazawa kunufaika kiuchumi.
Mhandisi Samamba alionya kuwa sekta ya madini inahitaji uwekezaji mkubwa, na pale wawekezaji wanapoweka mitaji yao, serikali haitawavumilia watoa huduma ambao si waaminifu au wanacheza na kazi zao. Aliitaka TAMISA kuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua wanachama wake wasiotimiza wajibu wao kitaaluma, akifananisha na jinsi Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) inavyoshughulikia wanachama wake wanaokiuka maadili. Aliahidi ushirikiano kamili kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Madini ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu na ubora wa huduma katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), Dkt. Theresia Numbi, alieleza kuwa mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na kutungwa kwa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018, vimeimarisha usimamizi wa masuala ya wazawa kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini. Alisema serikali ina jukumu la kuandaa na kusimamia programu zinazohimiza makampuni ya madini kununua bidhaa na huduma zinazotolewa ndani ya nchi na wazawa.
Dkt. Numbi alibainisha kuwa usimamizi makini wa Local Content umefungua milango mingi ya fursa kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na nafasi za ajira, mafunzo, uhamishaji wa teknolojia, utafiti, na matumizi ya bidhaa na huduma za ndani. Hii imefanya sekta ya madini kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwapa fursa za kukua kiuchumi na kiteknolojia. Alisisitiza kuwa Wizara ya Madini na Tume ya Madini zitaendelea kusimamia hili na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa bidhaa za ndani na huduma za wazawa.
Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, CPA Venance Kasiki, alitoa wito kwa wazawa kushirikiana na TAMISA kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la ndani la madini. Alisema ushirikiano huu utawawezesha wazawa kutumia maarifa yao ndani ya mfumo rasmi wa biashara, jambo litakalochangia maendeleo jumuishi. Aidha, alisema ushirikiano huo utasaidia kuanzisha miundombinu bora na huduma za kisasa zitakazosaidia hata wachimbaji wadogo kufikia viwango vya kimataifa, kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani, tija katika sekta, na hatimaye kuongeza mapato ya serikali na ajira kwa wananchi.
Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalila, alisema matarajio yao ni kuona thamani ya Shilingi Trilioni 3.1 inayotajwa kama fursa ya local content kwa watoa huduma migodini, inanufaisha Watanzania moja kwa moja. Aliahidi kuwa TAMISA itafanya mchujo wa mara kwa mara kwa wanachama wake ili kuhakikisha wanaaminika na kuepuka kuharibu kazi wanazopata migodini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA, Dkt. Sebastian Ndege, alisisitiza kuwa kutokana na utajiri wa madini nchini na uwekezaji unaofanywa na kampuni za ndani na nje, ni muhimu kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi huu. Alikiri kuwa wazawa wana haki ya kutoa huduma, lakini pia wana wajibu wa kutoa huduma bora, kwa wakati, na kwa weledi wa hali ya juu. Aliahidi kuwa TAMISA itasimamia wanachama wake kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma ili kujenga uaminifu.