Katika jamii yetu, kuna viumbe wengine ambao huogopwa na mara nyingi huonekana kuwa hawana umuhimu mkubwa. Nyoka ni mmoja wao. Viumbe hawa wenye sifa mbalimbali, ingawa huogopwa na binadamu wengi, wana nafasi muhimu sana katika mfumo wa ikolojia duniani. Kuelekea Siku ya Nyoka Duniani itakayoadhimishwa Julai 16, 2025, tunakuletea mfululizo wa taarifa muhimu kuhusu viumbe hawa wa ajabu.
Tito Lanoy, mkufunzi kutoka Chuo cha Uhifadhi Wanyamapori cha Afrika (Mweka) na pia Mwanzilishi na Rais wa Tanzania Jamii ya Wataalamu wa Nyoka Tanzania, ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu historia na tabia za nyoka, ikiwemo uwezo wao wa kujilinda kwa kutoa sumu au kubadilisha rangi. Lanoy ameeleza kuwa nyoka ni miongoni mwa viumbe vya kale zaidi duniani, na wametukuzwa katika hadithi na tamaduni mbalimbali duniani kote, zikionyesha hekima na nguvu zao za ajabu.
"Kufikia sasa, kuna aina takribani 4,038 za nyoka duniani," alisema Lanoy. "Wanapatikana kuanzia kwenye baridi kali ya kaskazini mwa Canada, hadi kwenye misitu ya mvua ya maeneo ya Ikweta, na hata kwenye bahari nyingi duniani." Akifafanua zaidi, aliongeza kuwa kati ya aina hizo, ni nyoka 725 tu ndio wenye sumu, na kati ya hao, ni aina 250 pekee ndizo zenye sumu kali inayoweza kuhatarisha maisha ya binadamu. Hii ina maana kuwa idadi kubwa ya nyoka hawana madhara kwa binadamu.
Lanoy alisisitiza kuwa nyoka ni wawindaji hodari sana, na huchangia pakubwa katika kudumisha usawa wa mfumo wa ikolojia. Kwa mfano, wanasaidia kudhibiti idadi ya panya na wadudu wengine hatari kwa mazao na afya ya binadamu. "Cha kuvutia zaidi ni kuwa nyoka ni viumbe wa enzi za kale, na hutupatia mwanga juu ya maisha ya nyakati za kabla ya historia, wakati ambao dunia ilitawaliwa na reptilia wakubwa," alieleza Lanoy.
Alitaja baadhi ya nyoka wanaovutia watu zaidi duniani kote, wakiwemo King Cobra, ambaye ni nyoka mkubwa zaidi mwenye sumu duniani na anafahamika sana kupitia filamu mbalimbali. Mwingine ni Rattlesnake, anayejulikana kwa sumu yake kali kiasi kwamba baadhi ya jamii huamini kuwa watu hulazimika kunyonya sumu kutoka kwenye jeraha, ingawa hii haishauriwi kamwe kiafya. Pia alimtaja Chatu Reticulated, ambaye ndiye nyoka mrefu zaidi duniani na huua mawindo yake kwa kukaba.
Siku ya Nyoka Duniani iliwekwa kwa lengo la kuwaelimisha watu zaidi kuhusu nyoka na mchango wao mkubwa katika mazingira yetu. Ni fursa ya kuondoa hofu na dhana potofu, na badala yake kujifunza jinsi viumbe hawa wanavyochangia katika afya ya sayari yetu. Kwa mfano, nchini Tanzania, baadhi ya aina za nyoka, kama vile chatu, huonekana kama ishara ya bahati njema katika tamaduni fulani, ingawa wengi bado huwahofia. Ni muhimu kuelewa umuhimu wa kuhifadhi viumbe hawa kwa ajili ya kudumisha usawa wa asili na afya ya mazingira tunayoitegemea.