Katika anga la Tanzania, kuna viumbe wenye umuhimu mkubwa wa kiikolojia, lakini wanatajwa kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka. Hawa si wengine bali ni tumbusi, ndege wanaofahamika kwa kazi yao ya kipekee ya kusafisha mazingira kwa kula mizoga. Licha ya umuhimu wao, wanakabiliwa na tishio kubwa la kutoweka kutokana na sumu zinazowekwa kimakusudi kwenye mizoga, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mfumo mzima wa mazingira.
Kulingana na wataalam wa uhifadhi, tumbusi wanapotea kwa kasi ya kutisha, ambapo asilimia 60 ya vifo vyao husababishwa na sumu, hasa viuatilifu vya kilimo kama 'Carbofuran'. Haya mara nyingi hutumiwa na wafugaji wenye hasira, ambao hweka sumu kwenye mizoga ya mifugo yao iliyokufa kwa kushambuliwa na wanyama wakali kama simba na fisi, wakiwa na lengo la kulipiza kisasi. Kwa bahati mbaya, waathirika wakuu wa sumu hizi huwa ni tumbusi ambao hukusanyika kwa wingi kula mizoga hiyo. Tukio moja tu linaweza kuua mamia ya tumbusi kwa wakati mmoja, na hivyo kuathiri vibaya idadi yao.
Mbali na kulipiza kisasi, matumizi haya mabaya ya sumu yanachochewa pia na imani potofu kwamba viungo vya tumbusi vina nguvu za kiroho. Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kichwa au mguu wa tumbusi unaweza kuleta bahati au mali, jambo ambalo limechangia kuwepo kwa biashara haramu ya viungo vyao. Takwimu zinazotisha zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2025, matukio zaidi ya 21 ya matumizi ya sumu yamerekodiwa nchini Tanzania, na kusababisha vifo vya tumbusi zaidi ya 1,000, ambapo wengi wao walikatwa vichwa. Hali hii haishii tu kwa tumbusi; pia imesababisha vifo vya simba 15, fisi saba na wanyama wengine, ikionyesha athari mbaya kwenye mfumo wa ikolojia kwa ujumla.
Wataalam wanasema kwamba athari za kupotea kwa tumbusi zilionekana wazi nchini India miaka ya 1990, ambapo idadi ya ndege hao iliporomoka kwa zaidi ya asilimia 99. Janga hili lilisababisha kuongezeka kwa mizoga, kuenea kwa magonjwa, kuongezeka kwa idadi ya mbwa wa mitaani na vifo vya mamia ya maelfu ya watu kutokana na magonjwa, ikiwemo kichaa cha mbwa. Serikali ya India ililazimika kutumia zaidi ya Dola bilioni 34 (sawa na takriban Shilingi trilioni 85 za Tanzania) kukabiliana na madhara hayo. Hili linatoa somo muhimu kwa Afrika, hasa Tanzania, ambayo ina aina nane za tumbusi, na zote ziko katika hatari ya kutoweka.
Kama suluhisho, Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeanza kuchukua hatua za kulinda ndege hawa. Mwaka 2023, ilizinduliwa Mpango wa Kitaifa wa Ulinzi na Usimamizi wa Tumbusi (2023–2033). Pia, wataalam wanapendekeza kupiga marufuku viuatilifu vyenye sumu kali, kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa tumbusi na kuvunja imani potofu. Usimamizi wa karibu wa uuzaji na matumizi ya viuatilifu unahitajika, na matumizi ya viuatilifu mbadala yaliyosalama kwa mazingira na binadamu yanahimizwa.