Serikali ya Tanzania imetangaza mkakati mpya na madhubuti unaolenga kukata mzizi wa fitina wa vifaa vya umeme visivyo na ubora vinavyoingizwa nchini na kuwasababishia wananchi hasara kupitia bili kubwa za umeme. Kuanzia sasa, kifaa chochote cha umeme hakitaruhusiwa kuingia sokoni bila kupitia vipimo vikali katika maabara mpya ya kisasa na kuthibitishwa kwa nembo maalum ya ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, alieleza kuwa hatua hii ni sehemu ya mapambano ya kitaifa dhidi ya upotevu wa nishati ya umeme. Alifafanua kuwa jitihada hizi zimefanikiwa kupunguza upotevu wa umeme kwenye gridi ya taifa kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi asilimia 14 sasa, na lengo ni kufikia asilimia tisa kwa kudhibiti vifaa vinavyotumia umeme kupita kiasi.
Uzinduzi wa maabara hii ya kwanza nchini, unaofadhiliwa na Serikali kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), utakuwa mkombozi kwa mwananchi wa kawaida. Mhandisi Luoga alibainisha kuwa vifaa vitano vyenye matumizi makubwa ya umeme majumbani na viwandani—viyoyozi (AC), majokofu, televisheni, feni, na mota za umeme—vitakuwa vya kwanza kupimwa. "Lengo letu ni kuhakikisha Mtanzania anaponunua kifaa, anapata chenye ufanisi, kinachotumia umeme kidogo na kinachodumu, hivyo kupunguza gharama za maisha," alisisitiza Mhandisi Luoga.
Alitoa mfano wa mfumo wa nyota utakaotumika kwenye majokofu, akisema jokofu lenye nyota tano litatumia umeme mchache sana kugandisha ikilinganishwa na lile la nyota moja, jambo litakaloonekana moja kwa moja kwenye bili ya mteja. Mbali na kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama, mkakati huu utasaidia kupunguza presha kwenye gridi ya taifa, na hivyo kuwezesha umeme wa ziada uliookolewa kutumika katika maeneo mengine yenye uhitaji, ikiwemo viwandani, na kuchochea maendeleo.
Washirika wa maendeleo wameipongeza Tanzania kwa hatua hii muhimu. Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Gertrude Lyatuu, na Mkuu wa Ushirikiano wa EU, Marc Stalmans, kwa pamoja walisema kuwa matumizi sahihi ya nishati ni njia endelevu ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme na ni hatua muhimu kuelekea maendeleo ya kijani.