Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja nchini, Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imechukua hatua ya kuwafikia moja kwa moja wauzaji na wasambazaji wa bidhaa zake, ili kusikiliza maoni yao na kuboresha huduma katika sekta muhimu ya mifugo. Chini ya kaulimbiu "Huduma Bora za TVLA ni Haki ya Kila Mteja," uongozi wa Wakala umefanya ziara katika maduka mbalimbali jijini Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.
Akiongoza ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TVLA, Bi. Furaha Kabuje, alisema lengo kuu ni kujenga uhusiano imara na wadau, huku akisisitiza kuwa maoni yao ndiyo dira itakayoiwezesha TVLA kuboresha ubora na usalama wa bidhaa zake, hususan chanjo za mifugo ambazo ni muhimu kwa afya ya wanyama na uchumi wa wafugaji.
"Tumedhamiria kuhakikisha kila mfugaji na mteja wetu anapata bidhaa na huduma za viwango vya juu. Tumeamua kutoka ofisini na kuja kuwasikiliza ninyi ana kwa ana ili tuelewe changamoto zenu na maoni yenu ili tuweze kuyafanyia kazi mara moja," alisema Bi. Kabuje.
Kwa upande wao, wauzaji waliofikiwa walieleza kuridhishwa na hatua hiyo ya TVLA, wakisema inajenga lugha ya pamoja na kuimarisha imani kwa bidhaa za ndani. Walitoa pongezi za dhati kwa ubora wa chanjo zinazozalishwa na Wakala, wakisema zimekuwa na matokeo chanya kwa mifugo ya wateja wao.
Hata hivyo, hawakusita kutoa maoni ya kujenga. Waliiomba TVLA kuboresha zaidi mtiririko wa upatikanaji wa bidhaa ili zisikosekane madukani pindi zinapohitajika. Vilevile, walipendekeza kuwepo kwa njia rahisi na ya moja kwa moja ya mawasiliano na maofisa wa TVLA ili kupata taarifa sahihi na za haraka kuhusu bidhaa na huduma.
Akijibu hoja hizo, Bi. Kabuje aliahidi kuwa TVLA itayafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa, ikiwemo kuimarisha mifumo ya usambazaji na mawasiliano. Alisema Wakala itaendelea kushirikiana na wauzaji kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa za mifugo ili kuleta tija inayokusudiwa katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.