Kampeni ya Kitaifa ya Uchanjaji na Utambuzi wa Mifugo, iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeshika kasi rasmi mkoani Iringa, ikilenga kuchanja takriban ng'ombe laki nne kama sehemu ya mkakati wa kuwainua wafugaji kiuchumi na kufungua masoko mapya ya mifugo. Zoezi hili mkoani humo linaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede.
Akizungumza Julai 3, 2025, baada ya kushuhudia zoezi hilo katika maeneo ya Kijiji cha Kalenga na Shamba la Mifugo la Kibebe, Dkt. Mhede alisema kampeni hii ya miaka mitano ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maisha ya mfugaji. Lengo kuu ni kuhakikisha afya bora ya mifugo ili kuongeza thamani yake na kukidhi vigezo vya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Habari njema kwa wafugaji ni kwamba serikali imetoa ruzuku kubwa, na kufanya gharama za chanjo kuwa nafuu zaidi. Hili lilithibitishwa na mmoja wa wanufaika, Donard Luhavi, ambaye alisema, "Gharama ya chanjo imepunguzwa kutoka Shilingi 1,000 hadi 500 kwa kila ng'ombe. Hii imetupa motisha mkubwa wa kushiriki kikamilifu."
Uongozi wa Mkoa wa Iringa umepokea kampeni hiyo kwa mikono miwili. Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Kheri James, alihakikishia wizara ushirikiano kamili, akisema afya ya mifugo ni msingi wa uchumi na uhakika wa chakula kwa wananchi wengi wa Iringa. "Tunapongeza juhudi hizi za serikali. Tumejipanga kuhakikisha kila halmashauri inashiriki kikamilifu," alisema Kheri James.
Tayari mkoa umepokea chanjo za kutosha kwa ajili ya ugonjwa hatari wa Homa ya Mapafu kwa ng'ombe (CBPP), pamoja na chanjo za kuku dhidi ya Kideri, Mafua na Ndui. Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo wa Mkoa, Hamadi Mwansasu, timu za wataalamu zimesambazwa katika halmashauri zote kuhakikisha zoezi linafanikiwa.
Wadau muhimu wakiwemo Chama cha Wafugaji Mkoa wa Iringa na wamiliki wa mashamba binafsi kama Richard Philips wa Shamba la Kibebe, wameipongeza serikali na kuwahimiza wafugaji wenzao kuchangamkia fursa hiyo adhimu ambayo itapunguza vifo vya mifugo na kuongeza tija katika uzalishaji.