Historia mpya imeandikwa katika sekta ya nishati nchini. Sauti za majenereta zilizokuwa zikirindima mitaani na viwandani sasa zinatarajiwa kubaki kuwa kumbukumbu, kufuatia kauli nzito na ya matumaini iliyotolewa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi. Akiwa katika ziara ya kikazi kukagua 'moyo' wa uzalishaji umeme nchini, Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Waziri Ndejembi ametangaza rasmi kuwa Tanzania imepiga teke la mwisho kwa adui anayeitwa "Mgao wa Umeme".
Akiwa amesimama juu ya tuta la bwawa hilo linalotajwa kuwa ukombozi wa kiuchumi, Waziri Ndejembi alijionea kwa macho yake jinsi mitambo inavyochakata maji kuwa nishati, na kuhakikisha kuwa megawati 2,115 zinazozalishwa hapo zimeleta uthabiti usiotingishika katika Gridi ya Taifa.
"Hakuna Giza Tena, Taa Ziwake" "Nimefika hapa kujiridhisha na ninaondoka kifua mbele. Nataka Watanzania wajue kuwa JNHPP imekamilika na inafanya kazi kwa ufanisi wa asilimia 100. Kero ya mgao wa umeme sasa tumeizika rasmi. Uzalishaji huu mkubwa umetupa jeuri ya kuwa na umeme wa ziada," alitamka Waziri Ndejembi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haikufanya makosa kuwekeza mabilioni ya fedha katika mradi huo.
Hata hivyo, Waziri Ndejembi alibainisha kuwa kuzalisha umeme ni hatua moja, na kuufikisha kwa mwananchi ni hatua nyingine. Hivyo, serikali sasa imehamishia nguvu zake katika 'kusuka' upya miundombinu ya usafirishaji (transmission lines). Alitolea mfano ujenzi wa njia kuu ya umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, na njia nyingine mpya kutoka JNHPP kwenda Mkuranga, ambayo ni mahususi kwa ajili ya kulisha kongani za viwanda na Jiji la Dar es Salaam.
Uhai wa Miaka 100 na Utunzaji wa Mazingira Katika kile kinachoonekana kama mtazamo wa mbali, Waziri Ndejembi aligusia suala nyeti la maji. Alibainisha kuwa "injini" ya bwawa hilo ni maji yanayotiririka kutoka Mto Kilombero (asilimia 80) na Mto Ruaha (asilimia 20).
"Uhai wa mradi huu unategemea sana sisi wenyewe. Tukitunza vyanzo hivi vya maji kwa kushirikiana na Wizara za Maji, Maliasili na TFS, bwawa hili litaendelea kuwasha taa za Tanzania kwa zaidi ya miaka 100 ijayo. Hii ni mali ya wananchi, tuilinde kwa wivu mkubwa," alionya Ndejembi.
TANESCO na Uwekezaji wa Trilioni 13.5 Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Lazaro Twange, amefunguka kuhusu 'mkwanja' mrefu uliowekezwa kuboresha sekta hiyo. Twange amebainisha kuwa jumla ya Shilingi Trilioni 13.5 zinatumika katika miradi 41 inayoendelea nchini kote, huku miradi 35 kati ya hiyo ikijikita katika ujenzi wa njia za kusafirisha umeme.
Mhandisi Twange alitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kukatika kwa umeme mara chache. "Nataka nieleweke vizuri, hatuna mgao. Umeme upo mwingi wa kumwaga. Wananchi wakiona umeme umekatika na tumetoa tangazo, wajue ni matengenezo au maboresho ya miundombinu ili kuufanya uwe bora zaidi, siyo kwamba umeme hautoshi," alifafanua.
Nyuklia na Jua: Dira ya Kesho Katika kuonyesha kuwa Tanzania haibahatishi, TANESCO imeweka wazi mipango yake ya baadaye. Mbali na kukamilisha miradi ya umeme wa jua kule Kishapu (Megawati 50) na umeme wa maji Malagarasi (Megawati 49.5), shirika hilo limeanza kuelekeza macho kwenye nishati ya nyuklia.
"Tuko kwenye hatua za mwisho za maandiko ya awali na mazungumzo na wawekezaji kuhusu umeme wa nyuklia. Hii ni sehemu ya maagizo ya Rais kuhakikisha tunakuwa na vyanzo mseto vya nishati," alieleza Twange na kuhitimisha kwa kuwakaribisha wawekezaji wa viwanda kuja nchini kwa wingi, akisema "Umeme upo, karibuni mzalishaji."
Ziara hii ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya kuhakikisha nishati inakuwa kichocheo cha uchumi wa viwanda na ustawi wa jamii, huku Tanzania ikijipambanua kama 'Power House' ya Afrika Mashariki.