Kilio cha muda mrefu cha wakazi wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, kuhusu kero ya kukatika kwa umeme na nishati hiyo kuwa na nguvu ndogo (low voltage), kimepata msikilizaji na mwarobaini wa kudumu. Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetangaza "hali ya hatari" dhidi ya giza katika wilaya hiyo inayokuwa kwa kasi, huku ikishusha mikakati mizito ya dharura na ya muda mrefu.
Hayo yamejiri tarehe 29 Novemba, 2025, wakati Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, alipofanya ziara ya kustukiza na kikazi katika Mkoa wa Kitanesco wa Kigamboni. Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua 'moyo' wa umeme wa wilaya hiyo, Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Dege, na kutoa maagizo yanayopaswa kutekelezwa kwa kasi ya kijeshi.
Mwarobaini wa Haraka: Megawati 22 kutoka Mbagala Katika kile kinachoonekana kama 'huduma ya kwanza' kwa tatizo hilo sugu, Waziri Ndejembi amebainisha kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuja na suluhisho la papo kwa hapo. Mpango huo unahusisha ujenzi wa laini mpya ya kusafirisha umeme itakayochota Megawati 22 kutoka kituo cha Mbagala na kuzimwaga Kigamboni.
"Hatukuja hapa kupiga stori, tumekuja kutatua changamoto. TANESCO wamenihakikishia kuwa laini hii ya dharura italeta Megawati 22 kutoka Mbagala. Hii ni 'booster' kubwa itakayoongeza upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa Kigamboni wakati tukiendelea na mipango mikubwa," alisisitiza Waziri Ndejembi huku akionyesha kukerwa na adha wanayoipata wananchi.
Mpango Kabambe: Transfoma ya MVA 120 na Mwisho wa 'Low Voltage' Kigamboni, ambayo inatajwa kama 'New City' ya Dar es Salaam kutokana na miradi mikubwa ya makazi kama Dege Eco Village na Avic Town, imekuwa ikiteseka na umeme hafifu usioendesha vifaa vya kisasa. Akikata mzizi wa fitina, Waziri Ndejembi ameeleza kuwa serikali inaongeza nguvu katika Kituo cha Dege kwa kusimika transfoma kubwa yenye uwezo wa MVA 120.
Mbali na hilo, operesheni ya 'nyumba kwa nyumba' ya kuondoa kero ya umeme mdogo inaendelea. "TANESCO tayari wameanza kazi ya kuweka transfoma 93 mitaani ili kuondoa hali ya umeme mdogo. Lakini hatuishii hapo, kuna zoezi la kusimika transfoma nyingine 50 ambazo zitakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi, 2026. Hii itakuwa suluhisho la kudumu kwa wateja wetu," alifafanua Waziri.
Uongozi wa Wilaya na TANESCO Wajipanga Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Mikaya Dalmia, amepokea mikakati hiyo kwa mikono miwili. DC Dalmia amemshukuru Waziri kwa kufika 'site' na kuona uhalisia, akibainisha kuwa nishati ya uhakika ndiyo injini ya uchumi wa Kigamboni ambayo inategemea sana utalii wa fukwe na viwanda vidogo.
"Mheshimiwa Waziri, ziara hii ina matokeo chanya sana kwetu. Nikuahidi ushirikiano wa dhati kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Nawaomba wananchi wa Kigamboni wawe wavumilivu kidogo wakati mafundi wakiendelea na maboresho haya, kwani mambo mazuri hayahitaji haraka," alisema DC Mikaya.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO (Usambazaji), Mhandisi Athanasius Nangali, amesema shirika hilo limeingia kazini rasmi kuanzia sasa. "Maelekezo ya Waziri ni sheria. Tutafunga hizo transfoma na kuleta hizo Megawati 22 haraka iwezekanavyo. Kigamboni lazima iwake," alihitimisha Mhandisi Nangali.
Hatua hizi za Wizara ya Nishati zinatazamwa kama ukombozi kwa Kigamboni, eneo ambalo kijiografia lilikuwa likitegemea miundombinu chakavu, lakini sasa linaelekea kuwa kitovu cha kisasa cha makazi na biashara jijini Dar es Salaam.