Jijini Dodoma, ambako ndiko kitovu cha maamuzi ya nchi, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amefungua ukurasa mpya wa utendaji kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku akitoa onyo kali linalofanana na 'kadi nyekundu' kwa wakandarasi wote wenye tabia ya "kusuasua" katika utekelezaji wa miradi ya nishati.
Katika kikao kazi kizito kilichoketi Novemba 22, 2025, na kuwashirikisha vigogo wote wa TANESCO kuanzia ngazi ya taifa, kanda, hadi mameneja wa mikoa na wilaya, Waziri Ndejembi ameweka wazi kuwa serikali haitakuwa na muhali wala kupepesa macho kwa yeyote atakayekwamisha azma ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kung'ara kwa umeme.
Akizungumza kwa lugha ya kizalendo na yenye mamlaka, Ndejembi amesisitiza kuwa mageuzi yanayoendelea ndani ya TANESCO yameanza kuzaa matunda yanayoonekana kwa macho na kuongeza imani kwa wananchi. Hata hivyo, amebainisha kuwa "kazi bado mbichi" na inahitaji kasi ya duma ili kufikia malengo ya "Misheni 300".
"Ndugu zangu, umeme sio anasa tena, ni haki na ni uchumi. Serikali imewekeza fedha nyingi. Hivyo, nataka niweke wazi hapa, wakandarasi wote watakaoshindwa kwenda na kasi yetu, sheria itafuata mkondo wake. Hatutabembeleza uzembe wakati wananchi wanahitaji nishati ili waendeshe viwanda, mashine za kusaga na biashara ndogondogo," alisisitiza Ndejembi.
Waziri huyo kijana na machachari ameliagiza shirika hilo kuongeza ubunifu wa hali ya juu katika kuwaunganishia wateja umeme. Lengo lililowekwa mezani ni kuhakikisha wateja wapya milioni 1.7 wanaunganishwa kwenye gridi ya taifa kila mwaka. Hii ni idadi kubwa inayolenga kuhakikisha kuwa hakuna kijiji wala mtaa unaobaki gizani.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amewatoa hofu Watanzania akieleza kuwa shirika hilo limejipanga kimkakati kutekeleza miradi muhimu ndani ya siku 100 za utendaji wa Rais Samia. Alitaja kwa umahususi Mradi wa Kufua Umeme wa Jua wa Kishapu, uliopo mkoani Shinyanga, ambao umefikia asilimia 83 ya utekelezaji. Mradi huu unatajwa kuwa mkombozi mkubwa wa kuongeza megawati kwenye gridi ya taifa, ukitumia rasilimali ya jua ambayo inapatikana kwa wingi Kanda ya Ziwa.
"Tumejipanga vyema na tuko tayari kwa kazi. Mradi wa Kishapu ni mfano tu wa kasi yetu, na tutahakikisha lengo la wateja milioni 1.7 linafikiwa kwa wakati," alieleza Twange kwa kujiamini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, alitumia jukwaa hilo kumwagia sifa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake wa kutoa fedha za miradi mikubwa, akisema dhamira ya Rais ni kuona Tanzania inakuwa nchi ya viwanda inayojitegemea kienerjia.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Felchesmi Mramba, aliongeza kuwa TANESCO sasa inatekeleza miradi yake kwa viwango vya kimataifa (International Standards), jambo linaloifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na nchi jirani. Kauli hiyo iliungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Zuhura Bundala, aliyesisitiza kuwa wafanyakazi wa shirika hilo ni wazalendo na wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha taifa linapata nishati ya uhakika.
Kikao hicho cha Dodoma kinatazamwa kama kengele ya kuamsha ari mpya ndani ya sekta ya nishati, huku wananchi wakisubiri kuona matokeo ya maagizo hayo, hasa katika upunguzaaji wa kero za kukatika kwa umeme na kasi ya uunganishaji wa wateja wapya vijijini na mijini.