Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ametangaza rasmi kuwa Tanzania sasa ina umeme wa kutosha kukidhi mahitaji yake, akisema ni matokeo ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya kimkakati, hasa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ambalo peke yake linaingiza megawati 2,115 kwenye gridi ya taifa.
Kauli hiyo ya faraja kwa Watanzania imetolewa leo, Julai 10, 2025, baada ya Dk. Biteko kufanya ziara ya kikazi kukagua vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension, na Kinyerezi II jijini Dar es Salaam. Alisema changamoto za upatikanaji wa umeme zilizokuwepo katika baadhi ya maeneo sasa ni historia.
Dk. Biteko alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, akimtaja kama ndiye kinara aliyewezesha mapinduzi haya katika sekta ya nishati. Alisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali, ikiwemo kuidhinisha bajeti ya Shilingi trilioni 2.3 kwa Wizara ya Nishati, ndio umezaa matunda haya yanayoonekana.
‘’Nataka niseme mbele yenu, Rais Samia ndiye kinara wa haya yote. Amefanya uwekezaji ambao haujawahi kutokea kwenye sekta ya nishati kwa lengo moja tu: kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa," alisema Dk. Biteko.
Pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji, Dk. Biteko alilipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa maboresho makubwa katika utoaji huduma. Alisema sasa shirika hilo limekuwa na mwitikio wa haraka katika kushughulikia dharura na changamoto za umeme, huku akipongeza kuanzishwa kwa kituo cha miito ya simu kinachowahudumia wananchi bila malipo.
Ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na umeme wa ziada, Dk. Biteko alieleza kuwa serikali inapanga kuongeza uwezo wa kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 zilizopangwa awali hadi kufikia megawati 1,000.
Katika ziara hiyo, Dk. Biteko aliambatana na viongozi waandamizi akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kuashiria uzito unaopewa na serikali katika kuhakikisha sekta ya nishati inaimarika.