Bilioni 556 Zatua Chalinze-Dodoma: Ndejembi Awasha Moto TANESCO, Ataka 'Spidi' ya Kijeshi

economy | Thu Nov 27 2025


Bilioni 556 Zatua Chalinze-Dodoma: Ndejembi Awasha Moto TANESCO, Ataka 'Spidi' ya Kijeshi

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuziweka kando siasa za maneno na kujikita katika siasa za vitendo kwenye sekta ya nishati, huku Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, akitangaza ukombozi kamili wa nishati kwa mikoa ya Kanda ya Kati kupitia mradi mkubwa wa njia ya kusafirisha umeme.


Akiwa katika ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa njia kuu ya umeme yenye msongo mkubwa wa Kilovoti 400 (400kV) inayoanzia Chalinze mkoani Pwani hadi jijini Dodoma, Waziri Ndejembi ametoa maagizo mazito kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wakandarasi, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia kusuasua kwa mradi huo unaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 556.


Fedha za Ndani na Fahari ya Taifa Akizungumza wakati wa ukaguzi huo uliofanyika Novemba 27, 2025, Mhe. Ndejembi alibainisha kuwa mradi huo ni kielelezo cha uwezo wa Tanzania kujitegemea, kwani unatekelezwa kwa asilimia 100 kwa fedha za ndani (kodi za Watanzania). Hatua hii inalenga kuimarisha usafirishaji wa umeme kutoka vyanzo vikuu vya uzalishaji, ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), ili kufika makao makuu ya nchi na maeneo mengine kwa ufanisi.


"Hizi ni fedha nyingi sana za walipa kodi, Shilingi Bilioni 556 si mchezo. Niwaagize TANESCO, simameni kidete kumsimamia Mkandarasi. Hatutaki kusikia visingizio wala hadithi wakati wa makabidhiano. Tunataka kuona thamani ya fedha (Value for Money) na mradi ukamilike kwa viwango vya kimataifa na kwa wakati uliopangwa," alisisitiza Waziri Ndejembi kwa sauti ya mamlaka.


Aliutaka uongozi wa TANESCO kukaa meza moja na Mkandarasi haraka iwezekanavyo ili kuandaa Mpango Kazi mpya (Action Plan) utakaoruhusu ufuatiliaji wa hatua kwa hatua, akionya kuwa serikali haitapokea mradi uliojengwa "nusu nusu".


Uzalishaji Umeme Sasa Basi, Kazi ni Usafirishaji Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Lazaro Twange, amewatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa nishati. Mhandisi Twange ameweka wazi kuwa Tanzania imevuka hatua ya "kulia gizani" kutokana na upungufu wa uzalishaji, na sasa changamoto iliyobaki ni kusafirisha umeme huo mwingi unaozalishwa ili ufikie kila kona ya nchi.


"Tanzania kwa sasa inazalisha umeme wa kutosha na ziada ipo. Kazi kubwa inayofanyika sasa chini ya maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kujenga 'barabara' za umeme (transmission lines). Tumekamilisha vituo vikubwa vya kupokea na kupoza umeme (substations) hapa Dodoma na kule Chalinze. Hivi vituo ndiyo moyo wa kusukuma umeme kutoka JNHPP kwenda mikoa mingine," alifafanua Mhandisi Twange.


Dodoma: Njia Panda ya Umeme Afrika Mashariki Mradi huu wa Chalinze-Dodoma una umuhimu wa kipekee kijiografia na kiuchumi. Mhandisi Twange alibainisha kuwa kituo cha Dodoma (Zuzu) si tu kwa ajili ya kuwasha taa Ikulu na Bungeni, bali kimegeuka kuwa 'Hub' au njia panda kuu ya nishati.


"Kituo hiki cha Dodoma ndicho kinachotuunganisha na gridi ya nchi jirani ya Kenya (Kenya-Tanzania Power Interconnector). Hii ina maana kuwa tunajenga mfumo imara unaokidhi mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo, na kutuwezesha hata kuuza umeme nje ya nchi kwa ufanisi," aliongeza.


Waziri Ndejembi alihitimisha ziara hiyo kwa kuwahakikishia wananchi kuwa dhamira ya Rais Samia ni kuona nishati inakuwa kichocheo cha uchumi wa viwanda, kilimo cha umwagiliaji, na biashara ndogondogo, hivyo miradi hii ya kusafirisha umeme ni uti wa mgongo wa maendeleo hayo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.