Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, hususan wale wa maeneo yenye msongamano mkubwa ya Mbagala na Gongo la Mboto, wamepata habari njema itakayomaliza kilio chao cha muda mrefu cha kukatika kwa umeme. Serikali imetangaza rasmi kukamilika kwa mradi mkubwa wa upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Kinyerezi I Extension, hatua inayotajwa kuwa ni mwarobaini wa kero za nishati katika ukanda huo wa Pwani.
Habari hii ya matumaini imetolewa Desemba 11, 2025, na Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, wakati wa ziara yake maalum ya kukagua utendaji wa mitambo ya kufua umeme jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo iliyohusisha ukaguzi wa vituo vya Kinyerezi I na II, pamoja na Ubungo I, II, na III, Naibu Waziri alijionea hatua kubwa iliyopigwa katika kuimarisha gridi ya taifa.
“Leo tunatangaza rasmi kuwa 'testing' au majaribio yameanza na yanakwenda vizuri. Mradi wa Kinyerezi 1 Extension umekamilika na tumefanikiwa kufunga Transfoma kubwa yenye uwezo wa MVA 175. Hii si habari ndogo, ni ukombozi kwa wananchi wa Gongo la Mboto na Mbagala ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia adha ya umeme mdogo au kukatika mara kwa mara,” alieleza Mheshimiwa Salome kwa kujiamini.
Kiongozi huyo alibainisha kuwa hatua hii ni matunda ya dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kuchagiza uchumi wa viwanda na biashara ndogondogo. Alisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha 'Bongo' haiwi gizani tena.
Kwa upande wa kitaalamu, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bwana Lazaro Twange, ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu maboresho hayo. Ameeleza kuwa ongezeko la watu jijini Dar es Salaam limekuwa likienda sambamba na ongezeko la mahitaji ya nishati, jambo lililolazimu kufanyika kwa upanuzi huo wa haraka.
“Tumejipanga kimkakati. Pale Kinyerezi tumesimika mtambo (Transfoma) wa MVA 175 ili kuongeza nguvu ya uzalishaji. Lakini haijaishia hapo, ili kuhakikisha umeme huo unawafikia walaji wa mwisho bila shida, tumefunga transfoma nyingine yenye uwezo wa MVA 120 maalum kwa ajili ya maeneo ya Gongo la Mboto na Mbagala. Hii inamaanisha uwezo wetu wa kusambaza umeme sasa unaendana na kasi ya ukuaji wa makazi na biashara katika maeneo hayo,” alifafanua Bwana Twange.
Ufafanuzi huo wa Bwana Twange unakuja kama faraja kwa wafanyabiashara wadogo kama wenye saluni, wachomelea vyuma (welding), na viwanda vidogo vilivyopo Mbagala na Gongo la Mboto, ambao shughuli zao zimekuwa zikiathirika mara kwa mara kutokana na umeme usiotabirika.
Kukamilika kwa mradi huu ni ishara kuwa TANESCO sasa inahama kutoka kwenye kuzima moto wa matatizo na kuelekea kwenye utatuzi wa kudumu wa changamoto za miundombinu. Wakati majaribio yakielekea ukingoni, matarajio ni kuwa sikukuu za mwisho wa mwaka 2025 zitasherehekewa kwa mwanga angavu katika jiji la kibiashara la Tanzania.