Kuna ripoti kuwa China imerejesha ndege tatu za abiria aina ya Boeing 737 MAX kwenda Marekani, hatua inayokuja wakati vita vya biashara kati ya Washington na Beijing vikizidi kupamba moto. Inasemekana kuwa mamlaka za China zimetoa maelekezo kwa mashirika ya ndege nchini humo kutosipokea ndege za Boeing kutokana na mzozo huo.
Tovuti ya habari za fedha ya Barron's, ikinukuu jarida la masuala ya anga la The Air Current, iliripoti jana, Aprili 17, 2025, kwamba ndege hizo tatu aina ya 737 MAX ziliondolewa kutoka kituo cha ukamilishaji cha Boeing kilichopo Zhoushan, China, na kurejeshwa Seattle, jimbo la Washington nchini Marekani, ambako ndiko makao makuu ya utengenezaji wa ndege za Boeing.
Msingi wa tukio hili ni ongezeko la mivutano ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili makubwa kiuchumi. Chini ya utawala wa Rais Donald Trump, Marekani imechukua hatua kali. Mnamo Aprili 2, Trump aliweka ushuru wa forodha wa asilimia 34 kwa bidhaa za China. China ilijibu mara moja kwa kuweka ushuru kama huo kwa bidhaa za Marekani. Kisha, Aprili 9, Rais Trump aliongeza tena ushuru wa asilimia 50 juu ya ule wa awali. Ukijumlisha na ushuru wa asilimia 20 aliokuwa ameweka awali akilalamikia China kutozuia dawa za kulevya aina ya fentanyl kuingia Marekani, jumla ya ushuru wa Marekani unafikia asilimia 145. Kwa upande wake, China imejibu kwa kuweka ushuru wa asilimia 125 kwa bidhaa inazoagiza kutoka Marekani.
Zaidi ya hayo, inaripotiwa kuwa China pia imeweka vizuizi katika usafirishaji wa madini adimu (rare earths) nje ya nchi, ikiwa ni njia ya kushinikiza sekta za teknolojia ya juu na za kijeshi za Marekani.
Kampuni kubwa ya utengenezaji ndege ya Marekani, Boeing, imejikuta katikati ya mzozo huu. Sababu kamili ya kurudishwa kwa ndege hizo tatu za 737 MAX bado haijawa wazi. Inawezekana ni kutokana na maelekezo ya serikali ya China kwa mashirika ya ndege kutosipokea ndege hizo. Lakini pia, inawezekana kuwa ni uamuzi wa mashirika yenyewe kukataa kuzipokea kutokana na bei kupanda maradufu. Ushuru wa asilimia 125 unaotozwa na China unafanya bei ya ndege hizo kupanda kwa zaidi ya mara mbili ya bei yake ya awali, jambo ambalo linayafanya mashirika ya ndege ya China kuona ni afadhali kugeukia ndege za Airbus kutoka Ulaya. Hata bila maagizo rasmi, ushuru huo pekee unatosha kufanya mashirika ya ndege kusitisha kabisa biashara na Boeing.
Rob Stallard, mchambuzi kutoka Vertical Research Partners, alibainisha katika uchambuzi wake wa Aprili 17 kuwa ndege hizo zilikuwa zikisubiriwa na mashirika ya Xiamen Airlines na Air China, lakini mashirika hayo yalizikataa. Stallard aliongeza kuwa mara ya mwisho kwa Boeing kuwasilisha ndege nchini China ilikuwa Aprili 8, siku moja kabla ya Marekani kuongeza ushuru zaidi na kushadidisha vita vya biashara. Mchambuzi huyo amependekeza wawekezaji kuendelea kushikilia hisa za Boeing (Hold/Neutral) na ameweka lengo la bei ya hisa kuwa dola 146.
Boeing inakadiria kuwa China itahitaji takriban ndege mpya 9,000 za kiraia katika kipindi cha miaka 20 ijayo. Kampuni hiyo ilikuwa na lengo la kuuza nusu ya ndege hizo, huku nusu nyingine ikiuzwa na mshindani wake mkuu, Airbus. Hata hivyo, vita vya sasa vya biashara vinaweka malengo hayo ya Boeing katika hatihati kubwa.