Kumekuwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu hatari ya moto unaosababishwa na vifaa vya kuhifadhi chaji (power bank) katika usafiri wa ndege. Hii inafuatia madai kwamba 'power bank' ndio chanzo cha moto kwenye ndege ya Airbus A321 nchini Korea Kusini. Hata hivyo, mamlaka za eneo hilo hazijasema rasmi kuwa moto huo ulisababishwa na kifaa hicho.
Sambamba na hilo, ndege nyingine ya Air Busan ilishika moto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Gimhae nchini Korea Kusini mnamo Januari 28 mwaka huu, na kusababisha majeraha madogo kwa watu watatu. Wizara ya Uchukuzi ya Korea Kusini ilisema mnamo Machi 14 mwaka huu kuwa uchunguzi uligundua 'power bank' iliyoharibika ndio ilisababisha moto kwenye ndege hiyo. Inaripotiwa kuwa 'power bank' hiyo ilikuwa katika sehemu ya kuhifadhi mizigo juu ya kiti cha abiria, ambako moto ulianzia. Wachambuzi wanasema kuwa kifaa hicho kilionyesha dalili za moto, lakini haijulikani ni kwa nini betri ya 'power bank' iliharibika. Ni muhimu kuzingatia kuwa ripoti iliyotolewa ilikuwa ya uchunguzi wa muda mfupi tu, na ripoti kamili bado haijatolewa.
Marufuku ya 2016
Kwa miaka mingi sasa, mashirika ya ndege duniani kote yamepiga marufuku 'power bank' kubebwa kwenye mizigo inayokaguliwa (mizigo unayokabidhi kabla ya kupanda ndege) kwa sababu za kiusalama. 'Power bank' zina betri za lithiamu-ioni, ambazo zina uwezo wa kuzalisha joto kali na hata kusababisha mshtuko wa umeme. Kitaalamu, inatajwa kuwa ikiwa kuna kasoro yoyote ndani yake, huweza kusababisha hatari ya moto.
Kufuatia ushauri uliotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) tangu mwaka 2016, abiria wamepigwa marufuku kubeba betri zozote za lithiamu-ioni kwenye mizigo iliyokaguliwa kwenye ndege. Kutokana na moto uliozuka kwenye ndege ya Airbus nchini Korea Kusini, kampuni ya Air Busan imeanza kuchukua hatua za ziada za kiusalama kwa kutangaza kuwa abiria hawaruhusiwi tena kubeba 'power bank' kwenye mizigo yao ya mkononi. Kampuni hiyo inasema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya 'power bank' kupata joto.
Wakati huohuo, mashirika mengine ya ndege kama vile China Airlines na Thai Airlines pia yanatekeleza sheria kama hiyo. Scoot, shirika la ndege la gharama nafuu la Singapore Airlines, linatarajia kupiga marufuku matumizi na kuchaji 'power bank' kwenye safari zake za ndege kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Mnamo Februari 28 mwaka huu, serikali ya Korea Kusini ilitangaza kuwa abiria wanaosafiri kwa ndege za ndani wanapaswa kubaki na betri zao na chaji badala ya kuzihifadhi kwenye masanduku ya juu ndani ya ndege. Hatua hizi zote zinatokana na kuwepo kwa matukio ya moto, hata kwenye meli, ambayo yamesababishwa na betri za lithiamu hapo awali.
Mnamo Machi 2017, headphones za mwanamke zililipuka kwenye ndege kutoka Melbourne, Australia, kuelekea Beijing, na kusababisha jeraha usoni mwake. Ilielezwa kuwa mwanamke huyo aliamka baada ya kusikia 'headphone' zake zikilipuka, na mara moja akazivua na kuzitupa chini. Baada ya ajali hiyo, ilibainika kuwa ilisababishwa na hitilafu katika betri ya lithiamu-ioni. Hapo awali, safari ya ndege huko Sydney, Australia, ilisitishwa baada ya moshi kuonekana kutoka sehemu ya mizigo. Baadaye iligundulika kuwa betri ya lithiamu-ioni iliyohifadhiwa kwenye mizigo ndio ilikuwa imeanza kuwaka moto.
Jumuiya ya Huduma za Mazingira ya Uingereza ilisema katika ripoti yake ya mwaka 2022 kuwa kuna matukio 700 ya moto yanaripotiwa kila mwaka katika sehemu za kutupa taka, na mengi chanzo chake ni betri za lithiamu zilizotupwa. Betri za lithiamu-ioni zinaweza kulipuka ikiwa zimeharibiwa au kuvunjika. Betri hizi hazitumiwi tu katika 'power bank', bali pia katika vifaa vingine kama vile miswaki ya betri, vinyago, simu za mkononi na kompyuta mpakato.
Kujua Betri za Lithiamu
Betri za lithiamu aina ya BSLBATT zinatajwa kutoa nishati zaidi kwa matumizi ya juu kuliko betri za kawaida za asidi ya risasi. Pia, zinachaji haraka na zina ufanisi mkubwa, zinadumu na hazihitaji matengenezo ya mara kwa mara. Kiutendaji, betri hizi zinatajwa kuwa na nguvu inayoweza kutumika mara nane hadi kumi zaidi na kasi yake ya kuchaji ni ya juu sana. Pia, betri zake hutumika vyema zaidi zinapochajiwa hata kwa kutumia nishati ya jua, na hata zikiwa hazina chaji, zina uwezo wa kudumu kama zimechajiwa.