Mkoa wa Shinyanga, ambao kwa miaka nenda rudi umefahamika kwa jua lake kali na ardhi kame, sasa unageuza changamoto hiyo kuwa fursa ya kiuchumi itakayoliondoa taifa gizani. Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya nishati safi, Wilaya ya Kishapu imekuwa kitovu cha uzalishaji wa umeme wa jua, huku serikali ikimwaga kiasi cha Shilingi Bilioni 118 kuhakikisha mitambo inanguruma na kuingiza megawati kwenye Gridi ya Taifa.
Hayo yamebainika Novemba 28, 2025, wakati Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Bw. Peter Mahindi, alipoambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Lazaro Twange, kukagua maendeleo ya mradi huo ambao umefikia hatua za lala salama. Mradi huu unatajwa kama kielelezo cha utekelezaji wa Ilani na maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kulifikisha taifa kwenye uzalishaji wa Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Neema ya Fidia na Utulivu wa Jamii Akizungumza kwa niaba ya wana-Kishapu, DC Peter Mahindi amesema mradi huo umepokelewa kwa 'mikono miwili' na wananchi. Tofauti na miradi mingi inayokumbwa na migogoro ya ardhi, wananchi wa Kishapu wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kulinda miundombinu hiyo.
"Hapa Kishapu, mradi huu ni kama mtoto wetu. Wananchi zaidi ya 1,200 waliopisha eneo hili tayari wameingiziwa 'mpunga' wao wa fidia, hivyo hakuna manung'uniko. Wameelewa kuwa umeme huu si faida ya Shinyanga pekee, bali utawasha taa hadi mikoa ya jirani ya Geita, Mwanza na Simiyu. Huu ni ukombozi wa kiuchumi kwa Kanda ya Ziwa," alisisitiza DC Mahindi.
TANESCO Yatoa 'Deadline' ya Kufa na Kupona Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Lazaro Twange, hakuja Kishapu kwa ajili ya kutalii. Akiwa na faili la maagizo ya Rais ya 'Siku 100', ametoa agizo zito kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo. Mhandisi Twange ametangaza tarehe 15 Januari, 2026 kuwa ndiyo siku ya mwisho ya kukabidhi mradi, na hakutakuwa na mjadala wa nyongeza ya muda.
"Tumemshukuru Rais Samia kwa kutupatia Bilioni 118, fedha hizi si za mchezo. Hivyo, namwagiza mkandarasi ahakikishe ifikapo Januari 15, 2026, kazi iwe imekamilika. Hatutaki kusikia visingizio vya mvua wala jua. Kinyume na hapo, sheria itachukua mkondo wake," alionya Mhandisi Twange kwa sauti ya mamlaka.
Kutoka Megawati 4,000 Kuelekea 8,000 Twange alifafanua kuwa mradi wa Kishapu, ambao kwa sasa umefikia asilimia 84 ya utekelezaji, ni kiungo muhimu katika mkakati wa taifa wa nishati mchanganyiko (Energy Mix). Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha zaidi ya Megawati 4,000 kutokana na vyanzo vya maji na gesi, lakini kuongezeka kwa umeme wa jua kutaongeza uthabiti wa upatikanaji wa nishati hiyo, hasa wakati wa kiangazi.
"Kadri tunavyoongeza vituo vya kuzalisha umeme kama hichi cha Kishapu, ndivyo tunavyorahisisha kazi ya kusambaza umeme vijijini na viwandani. Umeme wa jua ni nafuu na rafiki wa mazingira, na hii ndiyo njia tunayoiendea sasa," aliongeza.
Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa TANESCO katika Kanda ya Ziwa imelenga kukagua miradi katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita na Kagera, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa hakuna mkoa unaobaki nyuma katika mapinduzi ya viwanda yanayotegemea nishati ya uhakika.
Mradi wa umeme wa jua wa Kishapu unatarajiwa kuwa mwarobaini wa kukatika kwa umeme mara kwa mara katika mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani, huku ukifungua fursa mpya za ajira na biashara kwa wakazi wa eneo hilo ambao awali walitegemea kilimo na ufugaji pekee.