Zaidi ya Wakulima 500 Shinyanga Wajadili Mikakati ya Kukuza Kilimo na Kuondokana na Umasikini

culture | Sat Apr 12 2025


Zaidi ya Wakulima 500 Shinyanga Wajadili Mikakati ya Kukuza Kilimo na Kuondokana na Umasikini

Zaidi ya wakulima 500 wa mazao ya chakula na biashara kutoka Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) 299 mkoani Shinyanga wamekutana kujadili mbinu mbalimbali za kukuza sekta ya kilimo ili iweze kuwanufaisha zaidi na kuwaondoa kwenye lindi la umasikini.


Wakulima hao, ambao wanatoka katika vyama vya msingi vinavyounda Vyama Vikuu viwili vya Ushirika mkoa wa Shinyanga – SHIRECU na KACU (Kahama Cooperative Union) – wamesisitizwa kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao yao ili yaweze kushindana katika masoko ya kimataifa.


Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa KACU, Bwana Emmanuel Nyambi, aliwakutanisha wakulima hao leo na kusisitiza kuwa kila mwaka wamekuwa wakikutana kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta ufumbuzi. Aliongeza kuwa changamoto ambazo zinazidi uwezo wao, huwasilishwa kwa wizara husika kwa hatua zaidi.


"Jukwaa hili limetukutanisha zaidi ya wakulima 500 kutoka vyama vya msingi 299 ili kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Tunaamini mikakati hii itawafanya wakulima kukua kiuchumi na kuondokana na umasikini," alisema Bwana Nyambi. "Ushirika ndio chombo pekee kinachowaunganisha wakulima wote nchini na kuwawezesha kunufaika na kilimo."


Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCu), Dkt. Gratian Rwekaza, alitoa mada kuhusu fursa za ushirika katika soko huria kwa ajili ya kukuza uchumi wa wanachama na jamii kwa ujumla. Aliwahimiza wakulima kulima kwa tija, kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato, na kuacha kutegemea ushuru pekee.


Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Bwana Kakozi Ibrahim, alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni "Ushirika hujenga ulimwengu ulio bora," na alieleza jinsi vyama vya ushirika vimekuwa vikisaidia wanachama wake kupata pembejeo na viuatilifu kwa wakati unaofaa.


Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Bwana Emmanuel Cherehani, aliwataka viongozi wa ushirika kufuata kanuni na sheria zinazoongoza ushirika, akionya kuwa baadhi ya viongozi wameshindwa kusimamia ushirika ipasavyo, kufanya maamuzi sahihi, na hivyo kusababisha migogoro.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi Anamringi Macha, aliushauri uongozi wa KACU kushirikiana kwa umoja ili kukifufua Chama cha Ushirika SHIRECU, ili kiweze kulipa madeni yake na kuanza kukopesheka na taasisi za kifedha kama ilivyokuwa hapo awali.


Pia, aliwataka wakulima wa zao la pamba kuacha mara moja tabia ya kuchanganya pamba mbegu na mchanga wakati wa masoko kwa lengo la kuongeza uzito. Alisema tabia hiyo inaharibu soko la kimataifa, inashusha bei, na inaipa nchi sifa mbaya ya kuwa na pamba chafu kila msimu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.