Vyama vya ushirika 299 kutoka Mkoa wa Shinyanga vimekutana katika Jukwaa la Ushirika la Mkoa, ambapo wameshauriwa kutumia vizuri fursa zinazotokana na mazao mbalimbali yanayolimwa katika eneo hilo kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Jukwaa hilo lilifanyika leo, na Mwenyekiti wake kwa mwaka huu ni Emanuel Nyambi, anayetoka Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kahama (KACU). Akizungumza katika jukwaa hilo, Bwana Nyambi alieleza kuwa jukwaa hilo limeanzishwa kwa mujibu wa sheria na linafanya kazi kihalali.
"Jukwaa hili limetukutanisha ili tuweze kuelezea changamoto mbalimbali zinazotukabili sisi na zinazoukabili ushirika kwa ujumla. Lengo ni kuzijadili kwa pamoja na kutafuta suluhisho la kudumu," alisema Bwana Nyambi.
Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCu), Dkt. Gratian Rwekaza, alitoa mada kuhusu fursa za ushirika katika soko huria kwa ajili ya kukuza uchumi wa wanachama na jamii kwa ujumla. Mgeni rasmi katika jukwaa hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi Annamringi Macha.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Bwana Ibrahim Kikozi, alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni "Ushirika hujenga ulimwengu ulio bora," na alieleza jinsi vyama vya ushirika vimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake kwa kuwapatia pembejeo za kilimo na viuatilifu.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Bwana Emanuel Cherehani, aliwataka viongozi wa ushirika kufuata kanuni na sheria zinazoongoza ushirika. Alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi wameshindwa kusimamia ushirika ipasavyo na kufanya maamuzi yenye utata. "Kama huna uwezo wa kusimamia ushirika, ndio unaosababisha ushirika kufa. Moja ya sifa za kiongozi ni kutunza siri za vikao, kuheshimiana, na kutoyumbishwa. Ukishindwa, utajikuta unafanya maamuzi kwa maslahi ya mtu mmoja na baadaye unakuwa gumzo kwenye vijiweni," alionya Bwana Cherehani.
Baadhi ya wadau waliohudhuria jukwaa hilo walitoa maoni yao. Meneja wa Agricom kutoka Wilaya ya Kahama, Bi Christina Mabula, alisema kuwa kampuni yao inatoa suluhisho la kumkomboa mkulima mmoja mmoja au vikundi vya wakulima. "Mpaka sasa, tumeweza kutoa matrekta 400 nchi nzima kwa kushirikiana na bodi ya pamba. Lengo letu ni kuwawezesha wakulima kuondokana na kilimo cha mazoea," alisema Bi Mabula.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya Global Leaf, Bwana Geofrey Pofia, alisema kuwa wamekuwa wakinunua zao la tumbaku kwa msimu wa pili sasa na wameingia kwenye ushindani ili kuhakikisha zao hilo linakuwa na tija kwa wakulima.
Meneja wa Benki ya Azani, Tawi la Kagongwa Wilaya ya Kahama, Bwana Dismas Wangwe, alisema kuwa benki yao imekuwa ikitoa mikopo kwa wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika, na fedha hizo zimekuwa zikirejeshwa kwa wakati baada ya kukopwa.