Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa takwimu za kushtua kuhusu hali ya afya ya kinywa na meno nchini. Imeelezwa kuwa asilimia 76.5 ya watu wazima kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea wanasumbuliwa na tatizo la kuoza meno, huku asilimia 31.1 ya watoto wakiwa na meno yaliyoanza kuoza.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo. Alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya afya ya kinywa na meno, ambayo yanatarajiwa kufanyika Mei 30 hadi 31, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Dk. Nzobo alisema kuwa magonjwa ya kinywa na meno ni miongoni mwa magonjwa yanayowasumbua Watanzania kwa kiwango kikubwa. Aliongeza kuwa pamoja na tatizo la kuoza meno, asilimia 67 ya watu wazima na asilimia 57 ya watoto wanasumbuliwa na magonjwa ya fizi.
"Changamoto nyingine ni kuwa na meno yaliyojipangilia vibaya. Asilimia 36 ya Watanzania wana changamoto ya meno yaliyojipanga vibaya," alieleza Dk. Nzobo.
Alisema kuwa Watanzania wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu namna sahihi ya kutunza afya ya kinywa na meno. Hali hii inasababisha idadi kubwa ya watu kupata matatizo mbalimbali ya kinywa na meno.
Dk. Nzobo alitoa mfano wa jambo ambalo watu wengi hawajui, ambalo ni namna sahihi ya kupiga mswaki. Alisema kuwa watu wengi hupiga mswaki na kisha kusukutua vinywa vyao kwa kutumia maji, jambo ambalo si sahihi. Alisema kuwa usahihi ni kutema povu la dawa ya meno bila kuosha kinywa kwa maji, ili kuacha dawa ya meno iendelee kulinda kinywa.
"Ili kukinga meno yako kutoboka, piga mswaki asubuhi baada ya kunywa chai na usiku kabla ya kwenda kulala kwa kutumia dawa ya meno. Ukimaliza kupiga mswaki, tema povu la dawa kisha sukutua mdomo kwa nje. Usisukutue ndani ya mdomo ili ile dawa iweze kuzunguka ndani ya kinywa chako kwa saa 12 na kutoa ulinzi wa meno," alishauri Dk. Nzobo.
Aliongeza kuwa matatizo ya meno yanaweza kutibiwa kwa njia mbalimbali, kama vile kuziba meno kwa muda mfupi au mrefu, tiba ya mzizi wa jino, kuondoa kiini cha jino, na kuondoa ncha ya mzizi wa jino.
"Ni baada ya njia hizi zote kushindikana ndipo kung'oa jino kunapaswa kuzingatiwa kama suluhisho la mwisho," alisema.
Dk. Nzobo alisema kuwa maonesho hayo ya afya ya kinywa yatasaidia kutoa elimu kuhusu afya ya kinywa na meno kwa Watanzania. Pia, yatatoa elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na bima za afya ili kupata huduma bora za matibabu ya meno, na kuhamasisha uwekezaji katika vifaa tiba vya kisasa kwa matibabu ya kinywa na meno.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Maonesho ya Afya ya Kinywa na Meno Tanzania, Dk. Ambege Mwakatobe, alisema kuwa maonesho hayo yatatoa nafasi ya kujifunza teknolojia mpya na kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali wa afya ya kinywa na meno.
"Maonesho haya ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kuongeza uwekezaji, na kuchochea ubunifu wa kiteknolojia ambao utaamua mustakabali wa sekta ya kinywa na meno nchini Tanzania," alisema Dk. Mwakatobe.
Maonesho hayo yanafanywa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za serikali na sekta ya afya, ikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Wizara ya Afya, Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania (TDA), na yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau wa sekta hiyo kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika.