Wanafunzi wa Kilakala Waililia Serikali Kuwekeza Kwenye Mafunzo kwa Vitendo

culture | Sat Mar 15 2025


Wanafunzi wa Kilakala Waililia Serikali Kuwekeza Kwenye Mafunzo kwa Vitendo

Jumla ya wanafunzi 123 kutoka Shule ya Sekondari ya Kilakala, iliyoko mkoani Morogoro, wameeleza haja kubwa ya serikali, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kutenga bajeti maalum itakayowawezesha kupata mafunzo kwa vitendo badala ya kujikita zaidi kwenye masomo ya nadharia pekee wanayopata darasani.


Wakiwa katika ziara ya kielimu kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Buzwagi, uliopo katika kata ya Mwendakulima, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wanafunzi hao walieleza kuwa mafunzo kwa vitendo ni muhimu sana katika kuimarisha uelewa wao na kuwapa ujuzi unaolingana na mahitaji halisi ya soko la ajira mara baada ya kumaliza masomo yao.


Consolata Ally, mwanafunzi wa kidato cha sita akisoma masomo ya Historia, Jiografia na Lugha (HGL), alieleza kuwa wengi wao wana shauku kubwa ya kujifunza kwa vitendo lakini wanakosa fursa hizo kutokana na changamoto za kiuchumi zinazowakabili wazazi wao pamoja na shule yenyewe. Hali hii inawafanya wategemee zaidi nadharia wanazopata darasani, jambo ambalo linaweza kuchangia matokeo duni katika mitihani yao na kuwafanya wengi wao kukosa ujuzi wa kujiajiri.


“Iwapo serikali itawekeza fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, taifa litanufaika kwa kuwa na wasomi wenye uelewa wa kina wa mambo wanayosoma, badala ya kukariri tu yale yaliyoandikwa kwenye vitabu. Mafunzo ya vitendo yanawapa wanafunzi picha halisi ya kile wanachojifunza darasani na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kazi,” alisisitiza Consolata.


Rebecca Masondowe, ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha sita, aliongeza kuwa kupitia ziara yao kwenye mgodi wa Buzwagi, wamepata uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira, baada ya kujionea kwa macho yao hatua mbalimbali za urejeshaji wa mazingira zinazofanywa na kampuni ya Barrick Buzwagi baada ya kusitisha shughuli zake za uchimbaji madini.


Mwalimu wa shule hiyo, Grace Moshi, alifafanua kuwa mwanafunzi ambaye amepata fursa ya kujifunza kwa vitendo ana uelewa mpana zaidi wa somo husika ikilinganishwa na yule ambaye amesoma kwa nadharia pekee. “Mwanafunzi anayesoma tu darasani anajaza maarifa kichwani bila kuwa na uzoefu halisi, hivyo anaweza kushindwa kujibu maswali ya mtihani kwa ufasaha. Lakini yule aliyepata mafunzo kwa vitendo, hata kama swali likija kwa namna gani, atakuwa na uwezo mkubwa wa kulijibu kwa usahihi kwa sababu ana uelewa wa kile anachokisoma,” alieleza Mwalimu Grace.


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Barrick Buzwagi, Stanley Joseph, alisema kuwa mgodi huo umekuwa ukipokea wanafunzi kutoka shule mbalimbali kwa nyakati tofauti ili kuwapa uelewa kuhusu shughuli za uchimbaji salama wa madini na athari zake kwa jamii na mazingira. “Tulisitisha uchimbaji wa madini mwaka 2019 na uchakataji mwaka 2021, lakini shughuli za kufunga mgodi kwa ujumla zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2027. Kwa sasa, tunafanya kazi ya kurejesha mazingira kwa kupanda miti na kuandaa eneo hili kuwa ukanda maalum wa kiuchumi. Halmashauri ya eneo hili itaendelea kunufaika kwa kupata mapato kupitia wawekezaji wapya watakaoanzisha shughuli zao hapa,” alisema Bwana Joseph.


Aliongeza kuwa lengo lao ni kuwaelimisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa sekta ya madini kwa uchumi wa nchi, akieleza kuwa karibu kila kitu tunachotumia, kikiwemo magari, saa, simu na vifaa vingine vingi, kinatokana na madini. Ziara hii imewapa wanafunzi wa Kilakala nafasi muhimu ya kujionea uhalisia wa sekta ya madini na kuimarisha wito wao kwa serikali kuongeza uwekezaji katika mafunzo kwa vitendo ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.