Neema ya Viwanda Ludewa: Shule ya Amali Mlangali Kuwa ‘Mkombozi’ wa Vijana, DC Thomas Afunguka Mazito

economy | Thu Dec 18 2025


Neema ya Viwanda Ludewa: Shule ya Amali Mlangali Kuwa ‘Mkombozi’ wa Vijana, DC Thomas Afunguka Mazito

Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya kimkakati ya kuwatoa vijana wa Wilaya ya Ludewa ‘kijiweni’ na kuwapeleka katika uzalishaji mali, anga ya elimu na uchumi mkoani Njombe inatarajiwa kubadilika sura kufuatia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ya Ufundi inayojengwa kwa kasi katika Kata ya Mlangali.


Mradi huu, ambao umekaa kimkakati jirani kabisa na eneo lililotengwa kwa ajili ya Kongani ya Viwanda (Industrial Cluster), unatajwa kuwa sulwaridi la kudumu kwa tatizo la ajira, ukilenga kuzalisha wahitimu ambao "hawabahatishi" sokoni bali wana ujuzi unaoanika fursa za ajira waziwazi.


Akifanya ziara ya ‘kushuka saiti’ kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Olivanus Thomas, amesema uwekaji wa shule hiyo jirani na viwanda si bahati mbaya, bali ni mpango mkakati (masterplan) wa kuhakikisha nadharia darasani inakutana na vitendo kiwandani.


"Hapa tunatengeneza daraja la moja kwa moja kutoka shuleni kwenda kazini. Vijana wetu watakaosoma hapa Mlangali hawatakuwa na haja ya kuzurura na vyeti kwapani wakitafuta kazi. Ukaribu wa shule hii na Kongani ya Viwanda utawapa fursa adhimu ya kujifunza kwa vitendo (practical training) na kuiva kistadi kabla hata hawajahutimu," amesema DC Thomas kwa msisitizo.


Amebainisha kuwa mradi huo ni kielelezo halisi cha utekelezaji wa Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhubiri injili ya elimu ya ujuzi ili kuliwezesha taifa kufikia uchumi wa viwanda.


"Dhamira ya Mhe. Rais ni kuona kijana wa Kitanzania anajitegemea. Hii shule itatoa 'pakeji' kamili; mwanafunzi anapiga kitabu cha darasani (elimu ya sekondari) huku mkono wa kushoto ukishika spana na nyundo. Akimaliza kidato cha nne, anatoka hapa akiwa fundi kamili anayeweza kujiajiri au kuajiriwa na viwanda vitakavyoibuka hapa Ludewa," alifafanua DC Thomas.


Kwa upande wa utekelezaji, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Bw. Castor Kibasa, ameeleza kuwa shule hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa wakazi wa Ludewa na Njombe kwa ujumla. "Hii ni fursa ya dhahabu. Jamii inayozunguka Mlangali itanufaika na mzunguko wa fedha, lakini kikubwa ni hawa watoto wetu kupata ujuzi adimu utakaolifanya soko la ajira liwatafute wao badala ya wao kutafuta soko," alisema Kibasa.


Akiwasilisha taarifa ya utayari wa mradi huo, Msimamizi Mkuu, Bw. Twalib Kavenuke, ametoa habari njema kwa wazazi na walezi, akibainisha kuwa "mzigo uko tayari" kwa ajili ya kuanza kazi.


"Tumejipanga kisawasawa. Serikali imeshaajiri walimu 14 waliobobea na tayari tumeshawapata wanafunzi 100 wa kwanza ambao watafungua dimba mapema mwaka 2026. Fani zitakazotolewa hapa ni zile zenye soko la uhakika kama vile umeme wa majumbani na viwandani, uchomeleaji vyuma (welding), ujenzi na ufundi wa matofali," alifafanua Kavenuke.


Aidha, kulingana na mwelekeo wa dunia katika nishati safi, Kavenuke ameongeza kuwa shule hiyo imepokea wataalamu wabobezi wa nishati ya jua (solar energy), hatua itakayowawezesha vijana wa Ludewa kuwa mstari wa mbele katika teknolojia hiyo inayokua kwa kasi.


Wilaya ya Ludewa, ambayo inasifika kwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya chuma na makaa ya mawe (Liganga na Mchuchuma), inahitaji kwa udi na uvumba wataalamu wa kada ya kati kama hawa watakaozalishwa Mlangali ili kuendesha uchumi wa viwanda unaotarajiwa kushika kasi mkoani Njombe.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.