Simanzi ya Psoriasis: Frank Alivyoteketeza Milioni 30 India Kupambana na 'Magamba' Mwilini

culture | Thu Dec 04 2025


Simanzi ya Psoriasis: Frank Alivyoteketeza Milioni 30 India Kupambana na 'Magamba' Mwilini

Katika jamii zetu za Kitanzania, kuna msemo usemao "kilio cha samaki machozi huenda na maji." Hii ndiyo hali halisi wanayopitia maelfu ya Watanzania wanaoteseka kimya kimya na ugonjwa wa Psoriasis. Wakati wengi wakidhani ni upele wa kawaida au mzio (allergy), kumbe ni "janga la kimya" linalotafuna ngozi, kuangua uchumi wa familia, na kuacha majeraha mazito ya kisaikolojia.


Frank Latamani, mkazi wa jijini Dar es Salaam, ni shahidi hai wa mateso haya. Kwa zaidi ya muongo mmoja, ameishi akipambana na ugonjwa huu sugu usioambukiza, ambao humfanya mtu atoke magamba na vidonda mwilini. Simulizi ya Frank si ya kawaida; ni safari ya maumivu iliyogharimu kiasi cha fedha ambacho kingeweza kujenga nyumba ya kifahari, yote ikiwa ni katika kusaka nafuu ya mwili.


Safari ya Maumivu na Gharama za Kutisha

Harakati za Frank, ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ulemavu wa Ngozi Tanzania (PSORATA), zilianza mwaka 2012 kama mchezo. Kilianza kiji-vipele kidogo kichwani na miguuni, lakini kadiri siku zilivyosonga, ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya. Mwaka 2016, mwili wake uliasi; ngozi ilibadilika rangi, michirizi ya damu ikaanza kutoka, na magamba yakatapakaa mwili mzima.


Baada ya kuzunguka hospitali mbalimbali nchini bila mafanikio ya kudumu, mwaka 2020 Frank alilazimika kupanda ndege kuelekea Hospitali ya Apollo nchini India. Safari hii haikuwa ya kitalii, bali ya kuokoa jahazi la uhai wake.


"Ilibidi ndugu na marafiki wachange. Tuliteketeza takribani Shilingi milioni 30 kwa ajili ya safari na matibabu hayo," anaeleza Frank kwa uchungu. Huko India, alipata dozi ya sindano mbili kwa wiki, ambapo kila sindano moja iligharimu zaidi ya Shilingi milioni 1.1. Piga hesabu ya haraka haraka, ni mtanzania gani wa kawaida anaweza kumudu gharama hizi?


Ingawa alirejea na nafuu fulani, janga la UVIKO-19 (Corona) lilipotua, lilimrudisha hatua kumi nyuma. Mlipuko huo ulipozuia safari za ndege na yeye mwenyewe kuugua Corona, hali ya ngozi yake ilirudi kuwa mbaya, ikimlazimu kuagiza dawa kwa gharama kubwa kutoka nje huku akiwa amekwama nchini. Kwa sasa, matumizi yake ya dawa kwa mwezi yanagonga takribani Shilingi 1,200,000, mzigo ambao ni mzito kwa mstaafu yeyote.


Aina za Psoriasis na Madhila Yake

Kitaalamu, Frank amepitia 'moto' wa aina tatu za ugonjwa huu:

1. Palmoplantar Psoriasis: Hii hushambulia viganja na nyayo, ambapo ngozi hubanduka kiasi kwamba mgonjwa hushindwa hata kushika kikombe au kutembea.

2. Inverse Psoriasis: Hujificha sehemu za maungio kama kwapani, kukiwa na wekundu na michubuko.

3. Plaque Psoriasis: Hii ndiyo huleta mabaka makubwa yenye magamba mgongoni na kifuani.


Kuna wakati Frank alishindwa hata kuoga au kuvaa nguo za kubana. "Maumivu yalikuwa makali kiasi kwamba kwenda msalani ilikuwa ni adhabu," anakumbuka.


Unyanyapaa: Kidonda Juu ya Kidonda

Mbali na maumivu ya nyama na mifupa, ugonjwa huu huja na 'kisu' kingine kikali: Unyanyapaa. Jamii inapoona mtu mwenye magamba, wengi hukimbia wakidhani ni ugonjwa wa kuambukiza. Frank anasema marafiki wengi walimtoroka.


"Unabaki wewe, familia yako na Mungu wako. Unajiona mzigo na thamani yako inashuka," anasema. Hali hii huwafanya wagonjwa wengi kupata msongo wa mawazo na wengine kutumbukia kwenye lindi la ulevi ili kupunguza machungu.


Kilio kwa Serikali na Bima ya Afya

Jolly Digallu, Mweka Hazina wa PSORATA na muathirika wa ugonjwa huo, anapaza sauti kwa niaba ya wanachama zaidi ya 300. Ombi lao kuu ni kwa Serikali na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuutazama ugonjwa huu kwa 'jicho la huruma'.


"Wengi wetu ni watu wazima, uwezo wa kifedha umeshuka. Sindano moja Shilingi 400,000 mpaka milioni, nani atamudu?" anahoji Jolly. Chama chao kimekuwa kimbilio la faraja, kikitoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa wanachama wanaojiunga baada ya kuthibitishwa na madaktari bingwa.


Kauli ya Mabingwa wa Afya

Dkt. Magdalena Dennis kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anafafanua kuwa Psoriasis inatokana na hitilafu ya kinga ya mwili (autoimmune disease) na wala si ugonjwa wa kuambukiza. Anasema katika kila wagonjwa 500 wa ngozi wanaofika Muhimbili, wawili huwa na tatizo hili.


"Tiba ipo ya kupunguza makali, lakini ni ghali sana. Changamoto kubwa ni uelewa mdogo; watu wanachelewa kufika hospitali wakidhani wamerogwa au ni upele wa kawaida," anasisitiza Dkt. Magdalena.


Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Psoriasis kila Oktoba 29, ujumbe kwa Watanzania ni mmoja: Tuache unyanyapaa, na serikali iingilie kati kupunguza gharama za matibabu haya ambayo kwa sasa ni mzigo usiabebeka kwa mwananchi wa kawaida.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.