Wakati mamilioni ya wanafunzi nchini Tanzania wakihitimisha mtihani wao muhimu wa darasa la saba wiki hii, hisia za furaha na ahueni kwa wazazi na walezi zinapaswa kuambatana na hali ya tahadhari ya hali ya juu. Kipindi hiki cha mpito, ambacho kwa wengi ni cha mapumziko, kwa bahati mbaya hugeuka kuwa msimu wa hatari kubwa kwa watoto, hasa wasichana, ambao huangukia kwenye mitego ya mila potofu na unyanyasaji unaokatisha ndoto zao ghafla.
Ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya jamii bado zinautazama mwisho wa elimu ya msingi kama mwisho wa safari ya kielimu kwa mtoto wa kike. Badala ya kuwapa fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari, wazazi na walezi hugeuka kuwa wasimamizi wa maangamizi ya maisha ya binti zao kwa kuwaingiza kwenye ndoa za mapema, kuwafanyia ukeketaji, au kuwatumbukiza kwenye ajira hatarishi. Wavulana nao hawako salama, kwani uhuru wa baada ya mitihani unaweza kuwasukuma kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya, uhalifu, na ajira hatarishi kama uvuvi na uchimbaji madini.
Takwimu zinaonesha picha ya kutisha. Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia ya Afya wa 2022, mikoa kama Arusha na Manyara inaongoza kwa asilimia 43 kwa vitendo vya ukeketaji, ikifuatiwa na Mara (asilimia 28) na Singida (asilimia 20). Vilevile, janga la mimba na ndoa za utotoni linazikumba kwa kasi mikoa ya Shinyanga (asilimia 59), Tabora (asilimia 56), na Mara (asilimia 55), kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Hii ni ramani ya aibu inayoonyesha jinsi tunavyoshindwa kama jamii kuwalinda watoto wetu.
Cha kushangaza na kuhuzunisha zaidi ni jinsi wazazi na ndugu wa karibu wanavyoshiriki kikamilifu katika kusababisha madhara haya. Ni wao ndio wanaogharamia sherehe za kuwaoza binti zao wenye umri wa miaka 14 au 15 kwa wanaume wanaowazidi umri kwa miongo kadhaa. Wanapokea mahari ya mifugo au fedha kama malipo ya "kumuuza" binti yao kwenye maisha ya mateso, vifo vya wakati wa uzazi, fistula, na matatizo ya afya ya akili. Hii ni biashara ya maisha ya mtoto inayofanywa na wale waliopewa dhamana ya kumlinda.
Wakati Tanzania ina sheria imara kama Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998, utekelezaji wake unakwamishwa na mila na desturi kandamizi. Baadhi ya kesi za unyanyasaji huishia kumalizwa kifamilia, huku wahusika wakiendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichotokea. Ni wakati sasa sheria hii itoe adhabu kali kwa wote wanaohusika, kuanzia wazazi hadi wale "waume" wanaonunua watoto.
Wajibu wa ulinzi haupaswi kuishia kwa watoto wa kuzaa pekee. Jamii inapaswa pia kuwakumbuka na kuwalinda wasichana wanaofanya kazi za ndani pamoja na watoto wa ndugu wanaoishi katika familia. Vitendo vya kuwanyanyasa, kuwanyima chakula bora, na kuwatenga ni ukatili unaopaswa kukemewa vikali. Hawa ni watoto pia, wenye haki na ndoto kama wengine.
Kwa hiyo, wito unakwenda kwa kila mzazi, mlezi, na mwanajamii: kumalizika kwa mtihani wa darasa la saba si mwisho wa jukumu lenu, bali ni mwanzo wa vita mpya ya kuhakikisha usalama na mustakabali mwema wa watoto wetu. Tuache kutumia fedha na nguvu zetu kuharibu maisha yao kupitia mila zilizopitwa na wakati, na badala yake tuwekeze katika elimu yao ambayo ndiyo ufunguo wa kuwakomboa kutoka kwenye lindi la umaskini.