MOTOSIBA Kahama: Vibanda Sita Vyateketea kwa Hitilafu ya Umeme, Mgodi wa Buzwagi Waokoa Hali

culture | Sun Oct 26 2025


MOTOSIBA Kahama: Vibanda Sita Vyateketea kwa Hitilafu ya Umeme, Mgodi wa Buzwagi Waokoa Hali

Jumla ya vibanda sita (6) vya biashara vimeteketea kwa moto, huku vibanda vingine saba (7) vikiokolewa, kufuatia hitilafu ya umeme iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Igalilimi Kata ya Kahama Mjini. Tukio hili limeweka taharuki kubwa kwa wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo.


Moto huo ulianza ghafla majira ya saa tatu usiku, huku moshi ukionekana ukipanda kutoka kwenye kibanda kimoja kilichokuwa kikiuza vifaa vya umeme kabla ya kuenea kwa kasi katika vibanda vya jirani.


Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Bw. Paul Hamka, ambaye duka lake lilikuwa karibu na eneo la tukio, amesema alipata taarifa za moto huo akiwa nyumbani kwake na kukimbia haraka kwenda kusaidiana na wananchi wenzake katika juhudi za kuzima moto na kuokoa mali kabla haujafika mbali.


Hamka ameeleza kuwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lilifika kwa wakati lakini walikumbana na changamoto ya kuishiwa maji. Walijaribu kutumia bomba la maji lililokuwepo karibu na maduka, lakini moto uliwazidi kutokana na ukubwa wake. Hali hiyo ililazimisha kuomba msaada kutoka kwenye Gari la Zima Moto la Mgodi wa Barrick Buzwagi, ambalo lilifika na kuongeza nguvu, na kufanikisha kuuzima moto huo.



Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, ASF Fatma Sato, alithibitisha kupokea taarifa za moto saa tatu usiku na kueleza kuwa walifika kwa wakati na kushirikiana na wananchi. Alibainisha kuwa moto ulikuwa mkubwa kutokana na baadhi ya vibanda kuwa na magodoro, vitambaa, nguo na maboksi, vitu ambavyo huwaka haraka. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakuna kifo wala majeruhi aliyepatikana, kwani wananchi walichukua tahadhari. Sato alithibitisha kuwa chanzo kikuu cha janga hilo ni hitilafu ya umeme.


Kutokana na hasara hii, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametoa wito mzito kwa wafanyabiashara wote mkoani humo kuchukua tahadhari. Amewataka kuhakikisha wanaweka vitambuzi vya moto (smoke detectors) na vizima moto (fire extinguishers) katika maeneo yao ya biashara. Mhita amesisitiza kuwa hatua hiyo ya kujikinga ni muhimu ili kuepuka hasara kubwa za mali na kuokoa maisha, akitumia kauli isemayo, "Kinga ni bora kuliko tiba."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.