Katika maadhimisho ya miaka 30 tangu mkutano muhimu wa Beijing kuhusu haki na maendeleo ya wanawake, Balozi Dk. Getrude Mongella ametoa wito kwa vyombo vya habari kote nchini Tanzania kubadilisha mtazamo wao. Badala ya kuwaonyesha wanawake kama watu dhaifu, anataka waonyeshwe kama nguzo muhimu za maendeleo katika jamii.
Akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 30 ya mkutano wa Beijing, Dk. Mongella alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la msingi la kuonyesha uwezo wa mwanamke katika nyanja zote za maisha. "Tunahitaji kuona wanawake wakionyeshwa kama wachimbaji madini wenye ujasiri, wahandisi wenye ujuzi, au wanawake wa vijijini wanaotoa tiba za asili. Tukishindwa kuonyesha picha hizi, tutaendelea kuwadhalilisha wanawake," alisema Dk. Mongella.
Akitoa tathmini yake kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Beijing, Dk. Mongella alieleza kuwa Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika kuwawezesha wanawake, hasa katika uongozi. Alitoa mfano wa kuwa na Rais mwanamke, akisema hii ni ushahidi kuwa wanawake wanaweza kushika nafasi za juu za uongozi.
"Katika elimu, tumefanya vizuri sana. Wasichana sasa wanapata fursa ya kusoma hadi elimu ya juu, na ari yao ni kubwa kuliko miaka ya nyuma," alisema. Pia, aliongeza kuwa katika uchumi, wanawake wengi wanajihusisha na biashara kwa ujasiri, tofauti na zamani ambapo walitegemea kuletewa mahitaji yao.
Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 ulikuwa muhimu kwa harakati za haki za wanawake duniani. Ulilenga kuwawezesha wanawake kisiasa, kiuchumi, na kijamii, na kupambana na ukatili wa kijinsia.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana, Dk. Mongella alisema bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kuhakikisha wanawake wana nafasi sawa katika jamii na sekta zote za maendeleo. Alieleza kuwa, vyombo vya habari vina jukumu la msingi katika kuonyesha mafanikio ya wanawake na kuhamasisha jamii kuwathamini na kuwapa fursa sawa.
Dk. Mongella aliongeza kuwa, ni muhimu kwa jamii kuondoa dhana potofu kuhusu wanawake na kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Alisisitiza kuwa, wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na wanapaswa kupewa nafasi sawa na wanaume.