Jina lake ni Gertrude, lenye asili ya Ujerumani likimaanisha "mkuki imara na wenye nguvu". Tafsiri hii ya jina inakidhi uhalisia wa maisha na utendaji kazi wa Balozi Gertrude Mongela, gwiji na mpigania haki za wanawake aliyekuwa Mwenyekiti na Mratibu wa Mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.
Mwaka huu, Balozi Mongela anatimiza miaka 80 ya uhai wake, huku akishuhudia miongo mitatu imepita tangu kuandaliwa na kufanyika kwa mkutano wa Beijing aliouongoza kwa umahiri mkubwa. Karibuni, "Mama Beijing" huyu alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu kwenye kongamano la kitaifa lililofanyika jijini Dar es Salaam, likiandaliwa na Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, kusherehekea miaka 30 na zaidi ya mafanikio ya Azimio la Beijing.
Akizungumza kwa hisia na ujasiri mkubwa, Balozi Mongela alifichua siri iliyowezesha kufanikiwa kwa mkutano ule wa kihistoria. Alisema ilikuwa ni lazima "kutunisha misuli" – kutumia ujasiri na nguvu kama maana ya jina lake – na kukataa kabisa kuzungumza na viongozi wa ngazi za chini. Badala yake, alisisitiza kukutana na kujadili masuala ya mkutano na Wakuu wa Nchi, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu au hata Wafalme, kwa kuwa ndiyo wenye mamlaka ya kufanya maamuzi, kupanga rasilimali, na kutoa baraka kwa utekelezaji.
"Nilikuwa jasiri na jeuri kwa makusudi," alisema Balozi Mongela kwenye jukwaa hilo la Dar es Salaam. Alifanya ziara mbalimbali duniani kote akikutana na viongozi wa juu pekee, akiamini kwa dhati kuwa ajenda ya mwanamke si suala dogo la 'katibu kata', bali ni ajenda ya juu inayohitaji ushiriki na maamuzi kutoka ngazi za juu kabisa za serikali na taasisi. Alitaja kukutana hata na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki wakati huo, Papa Yohana Paulo wa Pili, kujadili masuala nyeti kama utoaji mimba na uzazi wa mpango, akijua fika yatakuwa na mjadala mkali Beijing.
Alieleza kuwa maandalizi ya mkutano huo yalianza kwa kukusanya maoni na taarifa kutoka ngazi za chini kabisa (vijijini), kisha wilaya, kitaifa, na hatimaye kimabara. Hii ilihakikisha walipofika Beijing walikuwa na uelewa wa kina wa matarajio na changamoto za wanawake kutoka kila kona, yakiwemo maoni ya kina mama wa Kitanzania walioshirikiana naye kwa karibu sana tangu alipoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN wa wakati huo, Boutros Boutros-Ghali. Taarifa hizi ndizo zilizochambuliwa na kuunda Tamko na Azimio Kuu la Beijing (Beijing Platform of Action) lenye maazimio 12 muhimu yaliyokuwa dira kwa maendeleo ya wanawake duniani.
Balozi Mongela anakiri kuwa amezaliwa akiwa na roho ya upiganiaji haki. Alisimulia kisa cha utoto wake mwaka 1955, aliposikia Mwalimu Julius Nyerere akihamasisha harakati za TANU na uhuru Ukerewe, akatoroka nyumbani kwa siri na kupanda gari la wajumbe kwenda kwenye mkutano, akijificha ili asionekane lakini asikie. Tangu utotoni, alikuwa muulizaji maswali na mtetezi wa haki, akihimiza hata baba yake kushiriki kazi za nyumbani kama kuwasha moto.
Katika kongamano hilo la Dar es Salaam, alimpa kazi maalum Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Fedha Hamad Chande. Alimtaka arejee miradi yote mikubwa ya ukandarasi inayotolewa na serikali, na akokotoe ni kiasi gani cha fedha hizo za Kitanzania, zinazotoka Hazina ya Serikali na ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na kodi za akina mama wakulima, wajasiriamali wadogo kama wauza vitumbua, kimewafikia wanawake kama wakandarasi au wataalamu.
"Mtaniambia mmejenga hospitali, sawa. Lakini aliyejenga ni nani? Alipewa kandarasi na nani?" alihoji kwa msisitizo. "Tunaona majengo makubwa yanajengwa Dodoma. Nina wasiwasi sana kama kuna mwanamama hata mmoja amepata zabuni ya ujenzi mkubwa. Pesa hizi ni za Kitanzania, zimechangwa na wanawake pia, lakini zinaishia mikononi mwa wanaume, wakiwemo wageni kama Wachina. Wanawake wanataka kujua ni shilingi ngapi zimetufikia kwenye miradi hii?"
Aliendelea kuhoji juu ya fedha za bajeti ya kilimo, akisema ingawa wanawake wanasifiwa kwa kulima, inafahamika kiasi gani cha pesa hizo za miradi ya kilimo, au za kuongeza thamani ya mazao, zinawafikia wakulima wadogo wadogo wa kike na vikundi vyao. Alitolea mfano wa pamba inavyochukuliwa kuongezewa thamani na wanawake kubaki kununua tu kanga na vijora, akisema hali hiyo haileti furaha.
Balozi Mongela alihimiza wanaharakati wa wanawake kufanya kazi zaidi kuhakikisha Azimio la Beijing linatekelezwa kikamilifu Tanzania. Aliwataka kuangalia kwa makini Dira ya Maendeleo 2025-2050 kama imejumuisha kikamilifu masuala ya Beijing na kuweka maono ya wanawake ndani yake. Pia, aliwataka kuwahi Ilani za Uchaguzi za mwaka 2030 ili kuhakikisha usawa wa kijinsia na utekelezaji wa Azimio la Beijing vinaingizwa na kutekelezwa. Aliagiza Azimio hilo litafsiriwe kwa lugha rahisi na kufikishwa vijijini ili Watanzania wote, wanawake kwa wanaume, wafahamu wajibu wao na wajibu wa serikali katika kutekeleza masuala yake.
Akigusia shamrashamra za kutimiza miaka 80, Balozi Mongela alisema Septemba mwaka huu itatimia miaka 30 kamili tangu Mkutano wa Beijing. Atasherehekea siku yake ya kuzaliwa na miaka hiyo ya Beijing kwa pamoja na wadau wake kuanzia Julai 31, ikiwa ni Siku ya Mwanamke wa Afrika, hadi Agosti 3.
Moja ya hoja zake kali ilikuwa kupinga matumizi ya jembe la mkono. "Wanawake wasaidiwe kutumia teknolojia. Jembe la mkono likome! Kupanda kwa mkono basi! Wanawake wameumia, bibi zetu waliumia, mama zetu waliteseka... hata leo kizazi kinaendelea kuteseka. Hapana, jembe la mkono lazima likome," alisisitiza. Alipendekeza serikali na wadau wajenge "senta za matrekita" ambapo wanawake wanaweza kukodisha kulimia, na kulipa baada ya kuvuna. Pia, aliitaka serikali, kupitia Naibu Waziri Chande, kuwekeza katika kufundisha wanawake TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), kama ilivyowezekana kufundisha elimu ya watu wazima.
Alikumbusha falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ya kujitegemea na kuacha kupiga magoti kuomba misaada kila wakati. Akirejelea uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kuzuia misaada na kuweka ushuru mkubwa, Balozi Mongela alisema: "Hii inatukumbusha maneno ya Nyerere, 'Mjitegemee'. Waafrika hatuna mjomba! Tujitegemee! Kila kitu tunacho. Tunakwama wapi? Tusaidieni wanawake, taifa letu lijitegemee. Kama wanaume wenzetu wameshindwa kufikiri, tuwasaidie, wamekwama wapi?" Alisisitiza kuwa safari ya kujitegemea inahitaji kila Mtanzania ashiriki kikamilifu, na wanawake hawana budi kuwa mstari wa mbele.