Kiongozi wa ACT Wazalendo Azuiwa Kuzungumza na Abiria Mwendokasi, Ashikiliwa na Polisi

culture | Fri May 23 2025


Kiongozi wa ACT Wazalendo Azuiwa Kuzungumza na Abiria Mwendokasi, Ashikiliwa na Polisi

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, ameeleza kukasirishwa na hatua ya wafanyakazi wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kumzuia kuzungumza na abiria katika Kituo cha Mwendokasi cha Kimara. Kitendo hicho kilisababisha kushikiliwa na polisi kwa zaidi ya saa tano.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi Mbezi, Mchinjita alieleza kuwa alifika kituoni hapo kama abiria wa kawaida, akifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kununua tiketi. Hata hivyo, alizuiwa kuzungumza na wananchi waliokuwa wakisubiri usafiri.


“Nilifika kama abiria wa kawaida, nikiwa na nia ya kuzungumza na wananchi ili kupata uzoefu wao kuhusu huduma. Cha kushangaza, wafanyakazi wa Udart walinijia na kunizuia wakidai kuwa nahitaji kibali maalum ili kuzungumza na abiria,” alisema Mchinjita.


Alifafanua kuwa hali hiyo ilizua mvutano, ambapo wafanyakazi hao waliita polisi ambao walifika na kujaribu kumkamata kwa nguvu. Katika vurugu hizo, baadhi ya vitu vyake vya kibinafsi viliharibiwa, ikiwa ni pamoja na simu yake, na waandishi wa habari waliokuwa naye walilazimishwa kufuta picha na video walizokuwa wamechukua.


“Polisi walitufikisha Kituo cha Polisi Mbezi, ambako tulishikiliwa kwa muda mrefu bila maelezo ya wazi. Tulielezwa tu kuwa Udart walikuwa na taarifa kutoka serikalini kuwa mabasi mengine yalikuwa njiani, jambo ambalo halikuwa na msingi wakati wananchi walikuwa wamekaa kwa saa kadhaa bila kupata huduma,” alisema.


Mchinjita aliongeza kuwa hali aliyoishuhudia Kimara ilikuwa ya kusikitisha, ambapo wananchi walikuwa wakisubiri mabasi kwa muda mrefu bila kupata taarifa au msaada wowote wa haraka.


“Hali ya usafiri wa mwendokasi ni mbaya sana, kuna upungufu mkubwa wa mabasi kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuongeza mabasi au kuwapa fursa waendeshaji wa ndani ili kusaidia kupunguza msongamano,” alisema.


Alisema kuwa baadhi ya watu waliokabidhiwa jukumu la kusimamia mradi huo wameshindwa, na sasa hali ni mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya wananchi.


“Watu wanakanyagana, wanavunjika miguu, kuna msongamano mkubwa, na nusu ya magari hayafanyi kazi. Inaonekana kuna mambo ya kifisadi yanafichwa kwenye uendeshaji wa mradi huu,” aliongeza Mchinjita.


Alipoulizwa kama polisi walimfungulia kesi, Mchinjita alisema hawakufunguliwa mashtaka yoyote, na waliambiwa kuwa wataitwa tena kituoni ikiwa itahitajika.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.