Wakala wa Mabasi Yaendayo Kazi (DART) imefikia hatua muhimu kwa kusaini mkataba wa muda mrefu wa miaka 12 na Kampuni Binafsi ya Emorates National Group (ENG) kutoka Abu Dhabi. Mkataba huu unahusu ununuzi wa mabasi mapya 177 ambayo yatahusika na njia muhimu ya usafiri kati ya Kimara na Mjini jijini Dar es Salaam.
Urasmi wa mkataba huu ulifanyika hivi karibuni, na unahusu awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi. Utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mfumo wa PPP, yaani ubia kati ya sekta binafsi na serikali, ambapo ENG itakuwa mshirika mkuu wa DART katika kuendesha huduma hiyo.
Kusainiwa kwa mkataba huu kumekuja baada ya mchakato mrefu wa taratibu za kisheria na manunuzi, ambapo kampuni ya ENG ilifanikiwa kushinda zabuni mara mbili. Sasa, ni rasmi kuwa utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Ikumbukwe kuwa ENG ilishinda zabuni ya kwanza ya mradi huu mwaka 2017, wakati wa serikali ya awamu ya tano. Hata hivyo, utekelezaji ulichelewa kuanza. Mwaka jana, Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athuman Kihamia, alieleza kuwa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kwa sasa inatolewa na mtoa huduma wa mpito, kampuni ya UDART, ambayo inaendesha mabasi 110 kwa sasa.
Hadi sasa, haijafafanuliwa wazi ni lini hasa Kampuni ya ENG itaingiza mabasi hayo nchini kwa ajili ya kuanza kutoa huduma rasmi kwa muundo wa PPP kama ilivyokubaliwa katika mkataba. Wananchi wanasubiri kwa hamu kuona mabasi mapya yakianza kazi ili kuboresha usafiri katika njia hiyo yenye mahitaji makubwa.
Mradi wa mabasi yaendayo kasi ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kutumia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) katika miradi mbalimbali. Kwa sasa, kuna zaidi ya miradi 80 ya PPP inayosimamiwa na kituo maalum (PPC), kwa lengo la kutumia mitaji ya sekta binafsi kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, ikiwemo usafiri wa uhakika na wa kisasa kama huu wa mabasi yaendayo kasi.
Katika hatua nyingine, mnamo tarehe 9 Mei mwaka huu, kampuni ya UDART iliingiza basi moja la mfano la kisasa linalotumia gesi kwa ajili ya majaribio. Basi hilo limekuwa likifanya safari kati ya Morocco na Posta jijini Dar es Salaam. Inatarajiwa kuwa baada ya kipindi cha majaribio cha miezi mitatu, mabasi mengine 99 ya kisasa yataingizwa nchini kwa ajili ya kuongeza nguvu katika huduma za usafiri zinazotolewa na UDART.
Sambamba na juhudi hizi za kuongeza mabasi, kunaendelea ujenzi wa barabara za mwendokasi katika njia mbalimbali jijini, ikiwemo barabara zinazounganisha Posta na Tegeta, Mwenge na Ubungo, pamoja na upanuzi wa kipande cha barabara kutoka Kimara hadi Ubungo. Miundombinu hii inatarajiwa kuwezesha uendeshaji mzuri na ufanisi wa huduma za mabasi yaendayo kasi mara baada ya mabasi mapya kuwasili na kuanza kazi.