Klabu ya Yanga Sports Club, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imetangaza rasmi kumpata Kocha Mkuu mpya atakayewaongoza katika msimu ujao wa mashindano. Hata hivyo, klabu hiyo yenye maskani yake Jangwani, Dar es Salaam, imeweka wazi kuwa haitomtangaza hadharani kocha huyo hadi hapo zoezi zima la usajili litakapokamilika, kwani kocha huyo ndiye anayesimamia moja kwa moja shughuli hiyo muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alithibitisha kuwepo kwa kocha huyo mpya na mipango iliyopo. Alisema kazi ya kwanza kabla ya kuanza usajili ni kuandaa barua za kuachana na wachezaji ambao hawataendelea kuwa sehemu ya kikosi kwa msimu ujao, huku akitarajia barua hizo kuanza kutolewa wiki ijayo. Baada ya zoezi hilo, Kamwe alieleza kuwa watakaa mezani na wachezaji walioisha mikataba yao ambao wanawahitaji, ili kuwafanyia mazungumzo ya kuwaongezea mikataba.
Vyanzo vya kuaminika ndani ya Yanga vinaeleza kuwa baada ya mchujo mkali, klabu hiyo imebaki na majina mawili makuu ya makocha. Majina hayo ni pamoja na Julien Chevalier, raia wa Ufaransa, ambaye kwa sasa anaifundisha klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, na Rhulani Mokwena, raia wa Afrika Kusini, ambaye aliwahi kuifundisha klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco. Mmoja wao ndiye atakayetangazwa kuwa Kocha Mkuu mpya wa Wananchi.
Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi wa kutomtangaza kocha huyo mapema, Kamwe alisema: "Kocha Mkuu ameshapatikana, atakuja na baadhi ya watu kwenye benchi letu la ufundi. Tumeweka kando kumtambulisha kwa sasa kwa sababu tupo katika kipindi muhimu cha usajili. Tunataka kumshirikisha kikamilifu kwenye usajili ili isije ikawa baadaye, kama mambo yataenda tofauti, akasema hakushirikishwa. Sisi Yanga huwa tunawashirikisha makocha wetu ndiyo maana mara nyingi tunafanikiwa." Aliongeza kuwa Yanga watashirikiana naye bega kwa bega, na kazi hiyo ikishakamilika ndipo watakuja kumtambulisha rasmi kwa wanachama na mashabiki wote wa Yanga.
Kamwe alifafanua kuwa, awali Yanga ilikuwa na orodha ya majina ya wachezaji waliopendekezwa kusajiliwa, ambayo yalitokana na ripoti ya benchi la ufundi lililopita. Hata hivyo, waliona si busara kuendelea na mchakato huo kabla kocha mpya hajaweka mawazo, ushauri, na nguvu zake kwenye mchakato wa usajili. "Ukweli ni kwamba hatujaanza usajili rasmi. Yapo majina ya wachezaji tunayo kutoka ripoti iliyopita, lakini tukasema si busara kuendelea na usajili kabla kocha mpya hajaweka mawazo, ushauri na nguvu zake," alisisitiza Kamwe.
Aliwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kutokuwa na wasiwasi wowote, akisisitiza kuwa klabu hiyo mara zote huwa makini sana linapokuja suala la kuboresha kikosi. "Wanachama na mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi, mara zote sisi huwa makini sana linapokuja suala ya kuboresha timu yetu. Tutaanza na kubakisha wachezaji bora tuliokuwa nao, halafu tunaongeza wengine ili kuweza kufikia malengo ya msimu ujao," alisema Kamwe.
Akimalizia, Kamwe alitoa siri ndogo kwa mashabiki: "Nikuibieni siri ni kwamba, kocha wetu mpya anaifahamu vizuri Yanga, kwa hiyo haitomuwia vigumu. Ukiona mchezaji amebaki, ujue kocha anataka kumtumia. Ukiona ameondoka, ujue hamhitaji." Alisisitiza kuwa kufika wiki ijayo, wataanza kuwapa barua wale ambao hawahitajiki, huku wakianza mazungumzo na wale wanaotaka kuwaongezea mikataba. Usajili utaendelea chini ya uangalizi wa kocha mpya, ambaye anachukua mikoba iliyoachwa na Miloud Hamdi. Hii inaashiria msimu mpya wenye mikakati mipya na matarajio makubwa kwa upande wa Yanga.