Kamwe Asema Usajili wa Conte ni 'Kitulizo' Tu, Makubwa Yanakuja Yanga

sports | Mon Jul 21 2025


Kamwe Asema Usajili wa Conte ni 'Kitulizo' Tu, Makubwa Yanakuja Yanga

Baada ya kimya cha muda, Klabu ya Yanga inatarajiwa kuanzisha kimbunga cha matangazo ya usajili kuanzia leo, ambapo itaanza rasmi kuwaaga wachezaji inaowaacha na kisha kuanika "mashine" zake mpya. Tayari wamemtangaza kiungo Mguinea, Balla Moussa Conte, lakini Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema huo ni mwanzo tu.


Akizungumza na wanahabari, Ali Kamwe alitamba kuwa usajili wa Conte, uliotikisa nchi kutokana na vita yake na watani zao Simba, ni "kitulizo" tu kwa mashabiki na wala si usajili wao mkubwa zaidi msimu huu.


"Hii ya Conte tumeitangaza kwa sababu tumeona watu wamejisahau, tulitaka kwanza tuichangamshe nchi," alisema Kamwe. "Wengi wanadhani huu ndio usajili wetu mkubwa zaidi, lakini nataka niwaambie, bado sana. Usajili mkubwa zaidi unakuja. Huyu ni kama tumemtambulisha tu kuonyesha kwamba tuko kazini."


Kamwe alieleza kuwa ameshakabidhiwa kabrasha lenye orodha kamili ya wachezaji wanaoondoka, wanaobaki, na waliosajiliwa. Alisema zoezi la kuweka kila kitu hadharani litaanza leo na litaendelea hadi Agosti 3, mwaka huu, ambapo wataanza na "Thank You" kwa wanaoondoka, kisha watafuata walioongezewa mikataba, na kumalizia na wachezaji wapya.


Wakati Yanga ikijipanga kuanika wachezaji wake wapya, tetesi zinaendelea kuwahusisha na majina makubwa, ikiwemo uwezekano wa kumsajili aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala', pamoja na viungo kutoka Ivory Coast, Mohamed Doumbia na Celestine Ecua.


Kwenye orodha ya wachezaji wanaotarajiwa kupewa mkono wa kwaheri, majina ya nyota kama Khalid Aucho, Clatous Chama, na Jonas Mkude yanatajwa kuwa kwenye hatihati, huku Kennedy Musonda akiwa tayari amejiunga na klabu nyingine nchini Israel. Wengine wanaotajwa ni Yao Kouassi na Jonathan Ikangalombo.


Mashabiki wa Yanga sasa wamekaa mkao wa kula, wakingoja kuona ni 'mashine' gani nyingine nzito zaidi ya Conte zitatambulishwa Jangwani.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.