Baada ya kutawala soka la ndani kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo, uongozi wa Klabu ya Yanga umetangaza rasmi kuwa sasa nguvu na akili zote zinaelekezwa kwenye medani ya kimataifa. Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, amesema wana "deni" kubwa kwa mashabiki wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu ujao wa 2025/2026 ni lazima walilipe.
Akizungumza kwa hisia, Rais Hersi alisema ingawa uongozi wake umefanikiwa sana ndani ya nchi, bado hawajaridhishwa na matokeo yao kwenye mashindano ya CAF. Alikumbushia jinsi timu ilivyoishia kwenye hatua ya makundi msimu uliopita na kusema hali hiyo haitavumiliwa tena.
"Tumebakisha mwaka mmoja katika kipindi chetu cha uongozi. Tumefanya vizuri sana kwenye ligi, lakini bado tuna deni kwenye mashindano ya kimataifa. Msimu huu tutafanya usajili wa nguvu na kuelekeza nguvu zetu huko ili kuhakikisha tunalilipa deni hili kwa Wananchi," alisema Hersi kwa msisitizo.
Ili kutekeleza ahadi hiyo, Yanga tayari imeshakamilisha kwa asilimia 85 usajili wa wachezaji wapya. Afisa Habari wa klabu, Ali Kamwe, alifichua kuwa wamekuwa wepesi na wenye maamuzi ya haraka sokoni, wakiwazidi kete baadhi ya klabu ambazo zilikuwa zikiwawinda wachezaji hao. "Sisi tumefika na kumaliza kazi haraka wakati wengine bado wanajadiliana. Hilo nisifiche," alisema Kamwe.
Sambamba na usajili, Yanga imefichua sifa za kocha wao mpya ajaye, ikionyesha mabadiliko makubwa ya falsafa. Kamwe alisema klabu haitafuti tena makocha wenye majina makubwa yaliyojengwa miaka ya 1990, bali wanataka kocha wa kisasa mwenye "mawazo mapya" atakayeipeleka timu kwenye kiwango cha juu zaidi.
"Hatukuangalia CV ya kocha aliyetwaa ubingwa mwaka 1956 au 1996. Tunaangalia mahitaji ya kikosi chetu kwa sasa. Tunamleta kocha wa kiwango cha juu na wa kisasa, ambaye atakuja na mbinu mpya na kuipeleka timu yetu juu ya hapa ilipo," alifafanua Kamwe.
Ingawa jina bado ni siri, tetesi zinaelekea kwa kocha wa sasa wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Mfaransa mwenye umri wa miaka 44, wasifu unaoendana kabisa na maelezo yaliyotolewa na uongozi wa Yanga.