Meneja wa zamani wa Arsenal, Arsène Wenger, ambaye sasa ni Mkuu wa Maendeleo ya Soka Duniani katika shirikisho la FIFA, amejitokeza na kutetea vikali mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu, akiyaita "mashindano ya kipekee" na muhimu kwa maendeleo ya soka. Kauli hii inakuja kama jibu la moja kwa moja kwa kocha wa zamani wa Liverpool, Jürgen Klopp, ambaye hivi karibuni aliyakosoa mashindano hayo na kuyaita "wazo baya zaidi kuwahi kutokea."
Wenger alipingana waziwazi na maoni ya Klopp, akisema, "Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni yake, lakini mimi siungi mkono mtazamo wa Klopp." Alionyesha kujiamini akisema, "Ukiuliza klabu zote zilizoshiriki, nina hakika asilimia 100 zitakujibu kuwa zinataka kushiriki tena."
Aliongeza kuwa mashindano hayo yamepata uungwaji mkono kamili kutoka kwa timu, wachezaji, na makocha walioshiriki. Hata hivyo, Wenger alisisitiza kuwa jambo la msingi zaidi ni kama mashabiki wameyapenda mashindano hayo. "Swali la msingi ni je, mashabiki wamefurahia? Mahudhurio ya mashabiki uwanjani yalikuwa makubwa kuliko hata tulivyotarajia. Jibu liko hapo," alisisitiza Wenger.
Mbali na mjadala huo, Wenger alizungumzia pia maandalizi ya Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika Amerika Kaskazini, akigusia changamoto ya hali ya hewa. Alikiri kuwa joto kali lilikuwa tatizo katika baadhi ya mechi zilizopita za Kombe la Dunia la Klabu.
"Tuliona joto lilikuwa changamoto katika baadhi ya mechi," alisema Wenger. "Lakini tulichukua hatua kama kunyunyizia maji viwanja wakati wa mapumziko."
Aliongeza kuwa FIFA inatafuta suluhu za kudumu, akisema, "Mwaka ujao, kutakuwa na viwanja vingi zaidi vyenye paa. FIFA imewaagiza watafiti kuchambua athari za joto, na imeonekana kuwa joto la zaidi ya nyuzi joto 35 linaathiri uwezo wa wachezaji kukimbia kwa kasi (sprints). Ni lazima tujiandae kwa hili."