"Huu ni mpira wa miguu kweli? Sielewi kabisa." Haya yalikuwa maneno ya Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, akielezea kuchanganyikiwa kwake na changamoto za ajabu zilizokikumba Kombe la Dunia la Klabu la FIFA la mwaka 2025. Michuano hii, iliyokusudiwa kuwa majaribio ya Kombe la Dunia la 2026, imeacha ujumbe mzito kwa FIFA baada ya kugubikwa na joto kali, mvua za radi, uhaba wa mashabiki, msongamano wa magari, na viwanja visivyoridhisha.
Michuano hii iliyodumu kwa mwezi mmoja nchini Marekani ilifanyika katika viwanja vitano vitakavyotumika pia kwenye Kombe la Dunia la 2026, na hivyo kufichua wazi matatizo yanayohitaji kufanyiwa kazi haraka.
Hali ya Hewa ya Kuogofya
Hali ya hewa ilikuwa changamoto kubwa zaidi. Sheria za Marekani zinalazimisha mchezo kusimamishwa pindi radi inapotambuliwa ndani ya eneo la kilomita 16, na mchezo huruhusiwa kuendelea dakika 30 baada ya radi ya mwisho kuonekana. Hii ilisababisha mechi sita kucheleweshwa, huku michezo miwili, ikiwemo ule wa Chelsea dhidi ya Benfica, ikichelewa kwa zaidi ya saa mbili. "Kama mechi nyingi hivi zinasitishwa, basi hapa sipo mahali sahihi pa kucheza mashindano," alilalama Maresca.
Joto kali lilikuwa tatizo lingine. Jiji la New York lilishuhudia joto la nyuzi joto 39°C, huku hisia ya joto ikifikia zaidi ya 50°C. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba mbwa wa kunusa madawa ya kulevya huko Philadelphia ilibidi avalishwe viatu aina ya 'Crocs' ili kuzuia miguu yake kuungua kwenye sakafu ya zege. Kocha wa Juventus, Igor Tudor, alisema wachezaji wake 10 waliomba kutolewa uwanjani kutokana na joto kali.
Viwanja Vitupu na Tiketi za Utata
Licha ya kuwa maandalizi ya Kombe la Dunia, idadi ya mashabiki ilikuwa "nusu mafanikio." Wakati fainali kati ya Chelsea na PSG ilijaza watu 81,118, mechi kati ya Ulsan na Mamelodi Sundowns ilihudhuriwa na watu 3,412 pekee. Michezo minne ilikuwa na mashabiki chini ya 10,000. Sababu zilizotajwa ni pamoja na baadhi ya mechi kuchezwa mchana wa siku za kazi.
Mfumo wa uuzaji tiketi wa FIFA, maarufu kama 'dynamic pricing', ulizua mzozo mkubwa. Tiketi za nusu fainali kati ya Chelsea na Fluminense zilianza kuuzwa kwa Pauni 350 (kama Shilingi milioni 1.2) lakini bei ilishuka ghafla hadi Pauni 10 (kama Shilingi 34,000) kabla ya mechi, jambo lililowakasirisha walionunua mapema kwa bei ya juu.
Miundombinu na Viwanja Visivyoridhisha
Ukubwa wa nchi ya Marekani ulifanya usafiri kuwa mgumu. Kwenye uwanja wa fainali, ilibidi utembee kwa dakika 20-30 kutoka kwenye kituo cha treni hadi lango la uwanja. Nusu fainali kati ya Real Madrid na PSG ilichelewa kuanza kwa sababu timu zote mbili zilikwama kwenye foleni.
Kuhusu viwanja vya kuchezea, vingi viliandaliwa kwa ajili ya mpira wa miguu wa Marekani (NFL) wenye nyasi bandia. Ingawa FIFA iliweka nyasi za asili, muda mfupi wa maandalizi ulifanya viwanja vingi kuwa na ubora duni. Kocha wa Dortmund, Niko Kovač, alilalamika kuwa uwanja mmoja ulikuwa kama "uwanja wa gofu; nyasi fupi sana na kavu, haufai kwa soka la kasi."
Mchambuzi wa soka, Michael Brown, alihitimisha, "Haya yalikuwa majaribio muhimu kwa Kombe la Dunia 2026. Ni wazi kuna kazi kubwa ya kufanywa." FIFA na Marekani sasa wana mwaka mmoja tu kurekebisha changamoto hizi kabla ya ulimwengu kuwasili kwa ajili ya Kombe la Dunia.