Simba Yashusha 'Mashine' Kutoka Kombe la Dunia la Klabu, Neo Maema wa Mamelodi Atajwa

sports | Tue Jul 29 2025


Simba Yashusha 'Mashine' Kutoka Kombe la Dunia la Klabu, Neo Maema wa Mamelodi Atajwa

Klabu ya Simba imeweka wazi kuwa kuanzia leo, itaaza kutikisa nchi kwa kuanza kutambulisha wachezaji wake wapya mmoja baada ya mwingine. Na kama dokezo la kwanza, imefichua kuwa miongoni mwa nyota hao ni mchezaji aliyeshiriki Fainali za Kombe la Dunia la Klabu zilizomalizika hivi karibuni nchini Marekani.


Akizungumza kwa mbwembwe jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, aliwaambia mashabiki wa Msimbazi wakae mkao wa kula, kwani wakati wa kushusha "wanyama wakali" umewadia.


"Wanasimba wanafahamu kuwa timu yetu ina mchezaji aliyeshiriki Kombe la Dunia la Klabu lililofanyika nchini Marekani? Hii ina maana kuwa mmoja wa wachezaji wetu wapya alikuwa kwenye moja ya timu zilizocheza michuano hiyo mikubwa. Tega sikio, kuna mashine za maana zinakuja," alitamba Ahmed.


Ingawa Ahmed Ally hakuweka wazi jina la mchezaji huyo, taarifa za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali zinaelekeza jina moja kwa moja kwa kiungo mshambuliaji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Neo Maema. Mamelodi ilikuwa moja ya timu nne zilizoiwakilisha Afrika kwenye michuano hiyo, pamoja na Al Ahly, Wydad Casablanca, na Esperance.


Inaelezwa kuwa usajili wa Maema (29) umekamilika kimyakimya, lakini Simba wamechelewa kumtangaza kwa sababu ya kimkakati. Mchezaji huyo ndiye nahodha wa kikosi cha Afrika Kusini (Bafana Bafana) kinachojiandaa na michuano ya CHAN, ambayo ni kwa ajili ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani.


"Kama Simba wangemtangaza mapema, angehesabika kisheria kama mchezaji wao na hivyo angekosa sifa ya kucheza CHAN. Waliamua kumuacha atumikie taifa lake kwanza, na baada ya mashindano hayo, atatambulishwa rasmi Msimbazi," kilieleza chanzo chetu.


Maema anajiunga na Simba akiwa na wasifu wa kuvutia, akiwa amecheza mechi 120, na kufunga mabao 13 na kutoa asisti 14 akiwa na Mamelodi Sundowns, klabu aliyoisaidia kutwaa ubingwa wa ligi mara nne.


Huyu anatajwa kuwa si mchezaji pekee kutoka Mamelodi anayetua Simba, kwani pia wanahusishwa na beki wa kati wa klabu hiyo, Rushine De Reuck, usajili unaoonekana kusimamiwa kwa karibu na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.