Timu ya soka ya Katunda FC imeibukaBingwa wa mashindano ya Katambi U-17 CUP baada ya fainali kusisimua iliyochezwa Aprili 4, 2025, katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM). Ushindi huo ulikuja kwa njia ya mikwaju ya penalti, ambapo Katunda FC iliweza kuwafunga Busulwa Sekondari na hivyo kutwaa kombe la ubingwa pamoja na zawadi ya fedha taslimu Shilingi milioni moja za Kitanzania (TZS 1,000,000).
Mgeni rasmi katika fainali hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bw. Julius Mtatiro, ambaye alishuhudia mchezo mkali uliodumu kwa dakika 90 bila timu yoyote kufunga goli. Hali hii ilipelekea mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambapo Katunda FC walifanikiwa kupata penalti 4 dhidi ya 3 za Busulwa Sekondari, na hivyo kuandika historia ya kutwaa ubingwa huo.
Katika hatua nyingine, timu ya Ngokolo Sekondari iliweza kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo, ikiwaonyesha ushindani mkubwa washiriki wengine.
Mkuu wa Wilaya, Bw. Mtatiro, alitoa zawadi kwa timu zilizoshinda, akitangaza rasmi Ngokolo Sekondari kuwa mshindi wa tatu na kuwazawadia kiasi cha Shilingi laki tano (TZS 500,000). Busulwa Sekondari, walioishia katika nafasi ya pili, walipokea kitita cha Shilingi laki saba (TZS 700,000), huku Katunda FC, mabingwa, wakiondoka na Shilingi milioni moja (TZS 1,000,000) pamoja na kombe.
Bw. Mtatiro alimpongeza kwa dhati Bw. Katambi kwa kuendelea kuunga mkono michezo katika wilaya hiyo. Alisema kuwa kupitia mashindano kama haya, vipaji vingi vya vijana vimekuwa vikiibuliwa na kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza jitihada hizi kwa manufaa ya vijana na jamii kwa ujumla.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Hamisa Chacha, alieleza kuwa michezo ina nafasi muhimu katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Alimpongeza Mbunge Katambi kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza ilani hiyo kwa vitendo, akiongeza kuwa michezo ni sehemu muhimu katika kuimarisha afya za watu, kuibua vipaji miongoni mwa vijana, na hata kuunda fursa za ajira.
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Shinyanga (SHIDIFA), Bw. Sylevester Budete, naye alimpongeza Bw. Katambi kwa kuendelea kuandaa na kudhamini mashindano hayo. Alimuomba kuendeleza juhudi zake za kuinua mchezo wa soka na michezo mingine kwa ujumla katika mkoa wa Shinyanga. Alisema kuwa mchango wake ni muhimu sana kwa maendeleo ya michezo katika eneo hilo.
Baadhi ya vijana walioshiriki katika mashindano hayo walitoa shukrani zao za dhati kwa Bw. Katambi kwa kuwapa fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika mchezo wa soka. Walisema kuwa mashindano hayo yamewasaidia sana kujiamini na kuonyesha kile wanachoweza kufanya.
Mashindano ya Katambi U-17 CUP yalizinduliwa rasmi Februari 18, 2025, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, Bw. John Siagi, katika Uwanja wa CCM Kambarage. Jumla ya timu 16 za vijana wenye umri chini ya miaka 17 zilishiriki katika mashindano hayo yaliyojaa ushindani na msisimko.