Kufuatia msimu wa kiangazi uliowaacha bila taji lolote, Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, chini ya Mwenyekiti wake Mohamed "Mo" Dewji, imetoa maamuzi yake mazito, ikimpa tena kijiti kocha mkuu Davids Fadlu huku ikitangaza panga zito kwa wachezaji kuelekea msimu ujao.
Katika kikao kizito kilichowakutanisha Bodi ya Wakurugenzi na Bodi ya Washauri, maamuzi hayo yalipitishwa baada ya tathmini ya kina ya msimu uliopita, ambapo Simba ilikosa mataji yote iliyokuwa ikiwania – Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la FA, na Kombe la Shirikisho Afrika.
Licha ya ukame wa mataji, bodi ilionyesha kuridhishwa na kazi ya Kocha Fadlu, hasa katika eneo la ujenzi wa timu, nidhamu na mbinu. Hivyo, wameamua kumuongezea mkataba mpya baada ya ule wake wa awali wa mwaka mmoja kumalizika.
"Uongozi wa Simba umeonyesha kuridhishwa na utendaji wake... ingawa hatukuchukua taji, maendeleo ya kiuchezaji yalionekana," kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu.
Akithibitisha taarifa hizo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kocha mwenyewe alikuwa na nia ya kubaki. "Kocha anaitaka Simba, amekwenda mapumzikoni na atarejea mwishoni mwa mwezi huu tayari kwa msimu mpya," alisema Ahmed.
Hata hivyo, uamuzi wa pili na mkubwa zaidi ni kufanya usajili wa "kuvamia soko." Ahmed Ally alifafanua kuwa bodi imeweka mikakati ya siri ya kuboresha kikosi kwa kiwango kikubwa. Hii ina maana kuwa kutakuwa na wachezaji wapya wenye uwezo wa juu watakaosajiliwa, na wakati huo huo, wachezaji kadhaa ambao hawapo kwenye mipango ya kocha na wale walioshuka viwango watafungashiwa virago.
"Tumefanikiwa eneo la kujenga timu, lakini tumefeli kwa kukosa makombe yote. Mipango iliyopo ni kuhakikisha msimu ujao tunaongeza ubora wa kikosi ili kutwaa mataji," alisisitiza Ahmed, huku akiahidi kuwa orodha rasmi ya wanaoachwa na wanaosajiliwa itatolewa hivi karibuni. Mashabiki wa Simba sasa wanasubiri kwa hamu kuona sura mpya ya kikosi chao kwa msimu ujao.