Zama Mpya Msimbazi: Usajili Wote Msimu Huu ni Chini ya Fadlu Davids, Ahmed Ally Afunguka

sports | Sun Jul 20 2025


Zama Mpya Msimbazi: Usajili Wote Msimu Huu ni Chini ya Fadlu Davids, Ahmed Ally Afunguka

Klabu ya Simba imeweka wazi kuwa imebadilisha kabisa mfumo wake wa usajili, na kwa mara ya kwanza baada ya misimu kadhaa, usajili wote unaofanyika kwa ajili ya msimu mpya uko chini ya mapendekezo ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kwa asilimia mia moja.


Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alikiri kuwa hii ni hatua kubwa na ya kimkakati, tofauti na misimu ya nyuma ambapo mara nyingi walikuwa wakimaliza ligi bila kuwa na kocha mkuu, jambo lililowalazimu kufanya usajili na kumtafuta kocha kwa wakati mmoja.


"Hizi ni zama mpya Msimbazi. Kwa miaka mingi, mara nyingi msimu kama huu ulikuwa unatukuta hatuna kocha. Lakini sasa, kwa asilimia 100, tunafanya usajili kwa mapendekezo ya benchi la ufundi, hususan Mwalimu Fadlu Davids," alisema Ahmed.


Alifafanua kuwa mara tu baada ya ligi kumalizika, Kocha Fadlu aliwasilisha ripoti yake ya kiufundi. Katika baadhi ya maeneo, alitaja moja kwa moja majina ya wachezaji anaowataka, na katika maeneo mengine, alielezea wasifu na aina ya mchezaji anayemhitaji ili kuziba mapengo.


"Fadlu ameridhishwa na mipango ya klabu na ameamua kuleta 'wanajeshi' wake. Sisi kama uongozi hatujamuangusha. Wachezaji wote aliowahitaji tumewapata, na wengine tupo kwenye hatua za mwisho kabisa. Viongozi wetu wametapakaa nchi mbalimbali za Afrika kukamilisha dili hizi," aliongeza Ahmed.


Kauli hii ya uongozi imepata nguvu zaidi baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed "Mo" Dewji, kuthibitisha kuwa alikuwa na mazungumzo ya kina na kocha huyo. Mo Dewji alimpongeza Fadlu kwa kuiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF katika msimu wake wa kwanza, licha ya kuwa na kikosi kipya.


"Nimefurahi kuwa na mazungumzo ya maana na Kocha Fadlu. Msimu huu ulikuwa wa kujenga timu, na bado tukafika fainali. Chini ya uongozi wake, Simba imefika fainali yake ya pili ya kimataifa katika historia ya klabu," aliandika Mo Dewji, akihitimisha kwa kauli ya matumaini makubwa: "Simba haitazuilika msimu ujao."


Wakati huo huo, Ahmed Ally amewakumbusha mashabiki kuwa zoezi la kuwashukuru wachezaji wanaoondoka bado linaendelea na baada ya hapo, wataanza kuwatambulisha wachezaji wapya waliosajiliwa.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.